SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA KALI WATU WANAJIHUSISHA NA UTOROSHAJI MADINI- DKT. KIRUSWA







Dar es Salaam.  

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali Wachimbaji wote na wafanyabiashara wa madini ambao hawatafuata Sheria ya Madini na kujiingiza kwenye utoroshaji wa madini, ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni, kutaifisha mali zao na kutoruhusiwa kufanya tena biashara ya madini hapa nchini.

Amesema hayo leo Novemba 16, wakati akifungua Mkutano wa Viongozi na Kamati Tendaji ya Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Karemjee, Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kiruswa amesema kupitia uongozi mpya wa FEMATA, Serikali inatamani kuona kasoro ya utoroshaji wa madini kwa wachimbaji wadogo inakwisha sambamba na kuelimisha umuhimu wa ulipaji kodi kwa wachimbaji wadogo wanaowaongoza ili Serikali iweze kutekeleza ipasavyo miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii ambayo inatagemea kwa kiasi kikubwa makusanyo ya ndani kutokana na shughuli mbalimbali za uchumi ikiwa ni pamoja na shughuli za madini.

“Wizara isingependa kuona uwepo wa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara ambao siyo waaminifu, Serikali haitosita kuwachukulia hatua kali wachimbaji wote na wafanyabiashara wa madini ambao hawatafuata Sheria ya Madini ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni na kutaifisha mali zao” amesema Dkt. Kiruswa.

Ameeleza kuwa, mikakati iliyopo kwa Serikali ni pamoja na kuwapatia Wachimbaji Wadogo maeneo ya uchimbaji na kusaidia kufanya utafiti kwa bei ndogo yenye ruzuku ya Serikali kupitia Shirika letu la Madini Taifa (STAMICO). 

“Nitoe rai kwa Wachimbaji Wadogo nchini kuchangamkia fursa hiyo ya kufanyiwa utafiti wa uchorongaji na STAMICO kwa bei nafuu yenye ruzuku ya Serikali” amesisitiza Dkt. Kiruswa.

Vilevile, Dkt. Kiruswa amewataka kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kujenga na sio kulumbana na kujadiliana mambo ya msingi kwa kuwa shirikisho hilo ni la kibiashara na kwamba matarajio ya serikali ni kuona FEMATA inapiga hatua kubwa huku wanachama wakizika tofauti zao.

Katika hatua nyingine,  Dkt. Kiruswa kwa niaba ya Viongozi na watumishi wa Wizara ya Madini, ametoa pole kwa Wafanyabiashara wa Kariakoo, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali kwa ujumla kwa ajali iliyotokea jana tarehe 16 Novemba 2024, ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne katika Mtaa wa Congo na Mchikichi, Kariakoo Jijini Dar es salaam huku akipongeza juhudi za uokozi zinazoendelea na kuwaombea kukamilisha zoezi hilo salama na kuwaokoa ndugu zetu wakiwa salama.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahaya Samamba ameipongeza FEMATA kwa mabadiliko chanya yaliyoleta utulivu katika Sekta ya Uchimbaji Mdogo na kuainisha kuwa Serikali kupitia Wizara inaunga mkono juhudi za FEMATA na wachimbaji wadogo kwa ujumla.

Sambamba na hilo, Mhandisi Samamba ameilekeza FEMATA kufanya marekebisho ya Katiba ya Shirikisho hilo, kwa kuwa itasawaidia kugawa majukumu, kuanisha maono na mipango yao kwa maendeleo endelevu. 

Amesisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote ya wachimbaji ili kufanya shughuli zao za uchimbaji kwa tija ikiwa ni pamoja na kkuwapatia maeneo ya kuchimba pamoja na kuratibu mikopo nafuu kufuatia majadiliano mazuri na taasisi za kifedha na mabenki. 

Naye, Rais wa FEMATA John Bina amesema kuwa Mkutano huo wa FEMATA umelenga la kuwasaidia viongozi wa shirikisho hilo ili waweze kutimiza wajibu wao kwa ufanisi zaidi na hatimaye kuleta matokeo chanya huku akimhakikishia Naibu Waziri Dkt. Kiruswa kuwa Shirikisho hilo litaendelea na kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kutumia masoko na vituo vya ununuzi vya madini kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Vilevile, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini ikiwa ni pamoja na mazingira bora kwa wachimbaji wadogo.

Comments

Popular posts from this blog

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

HUU NDIO USHAURI WA TMA KWA SEKTA HIZI ...