ACT YAPINGA TAMISEMI KUSIMAMIA UCHAGUZI

 

Na Mwandishi wetu, Habari Plus

Chama cha ACT-Wazalendo kimesikitishwa na taarifa walipokea kutoka kwa msajili wa vyama vya siasa kuwataarifu kuwa Wizara Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) itaendelea kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu amesema wapokea barua ambayo inaeleza TAMISEMI inaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambapo Juni 15, 2024 itafanya kikao cha wadau kukusanya maoni ya rasimu ya kanuni zitakazosimamia uchaguzi huo.

Amesema kuwa kitendo cha Tamisemi kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa ni kuvunja sheria kwani kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Mwaka 2024, kinaeleza tume hiyo ndio  imepewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji. 

"Msimamo wa muda mrefu wa Chama chetu ni kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI ndiyo maana ACT Wazalendo tulishiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa Bunge linapitisha kifungu cha Sheria kuwezesha jambo hilo," amesema Ado

Ameongeza"Ni jambo la kusikitisha kuwa Serikali hadi leo inasuasua kupeleka muswada Bungeni kutekeleza matakwa haya ya Sheria na badala yake inataka kuvunja Sheria kwa kuipa madaraka TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa,".

Amesema kuwa, hatua yoyote inayochukuliwa na TAMISEMI hivi sasa kuhusiana na usimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni batili na ni kinyume na sheria.

Akieleza kuhusu msimamo wa ACT Wazalendo, ameeleza watakwenda kwenye kikao cha wadau kilichoitishwa Juni 15, 2024 Dodoma kuieleza TAMISEMI isimamishe mara moja michakato inayoendelea nao wa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu ni batili na unavunja sheria za nchi.

Katika kuhakikisha hawakubalinia na uamuzi huo, chama hicho wamewasiliana na Asasi za Kiraia juu ya umuhimu wa kufungua kesi mahakamani kuzuia hatua za maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinazoendelea kuchukuliwa na TAMISEMI. 

"Tumefarijika kuwa Asasi hizo zipo kwenye hatua za mwisho kufungua kesi hiyo. ACT Wazalendo itatoa ushirikiano kwa taasisi hizo kwenye kesi hiyo" amesema Ado.

Sambamba  na hayo amebainisha kuwa kufuatia hali inayoendelea na kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, wataandaa kikao maalum na kuvialika vyama vingine vya siasa kuweka msimamo wa pamoja juu ya kuizuia TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia kuteuliwa wajumbe wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi ili wachukue nafasi ya waliopo sasa kwa mujibu wa sheria, ambao ndio waliovuruga uchaguzi wa 2020.

Comments

Popular posts from this blog

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

HUU HAPA MWENENDO WA KIMBUNGA "HIDAYA" , UPEPO KUVUMA KWA KASI YA KILOMITA 130 KWA SAA

NHIF YAFANYA MABORESHO YA KITITA CHA HUDUMA ZA MATIBABU, YAENDELEA KUPOKEA MAONI