JAJI MLACHA - WANANCHI KIGOMA HAWATAKI USULUHISHI
Na mwandishi wetu, HPMedia, Kigoma
IMEELEZWA kuwa kati ya mashauri 5366 yaliyofunguliwa kwenye mahakama za mkoa wa Kigoma ikiwemo Mahakama Kuu hadi za mwanzo kwa mwaka 2022 ni mashauri 256 tu yaliyomaliza kwa njia ya usuluhishi ambayo ni sawa na asilimia 4.8 tu ya mashauri yaliripotiwa na yaliyobakia yamemaliza kwa njia hukumu.
Kauli hiyo imetolewa leo mkoani humo na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Lameck Mlacha katika hafla ya kuhitimisha wiki ya sheria ikiwa ni ishara ya ufunguzi wa shughuli za mahakama kwa mwaka 2023 ambalo amesemawananchi wengi hawataki kesi zao kuishiakwa njia ya usuluhishi.
"Mkoa wa Kigoma unakabiliwa na changamoto kubwa ya kuamua mashauri kwa njia ya usuluhishi kutokana na wananchi wengi mkoani Kigoma kutotaka kesi zao kuisha kwa njia ya usuluhishi badala yake kutaka mashauri yao kutolewa hukumu na Hakimu au Jaji"amesema Jaji Mlacha.
Amesema kuwa, miongoni mwa sababu zinazopelekea kukwama kwa mashauri mengi na kuamuliwa kwa njia ya usuluhishi ni kukosena kwa utayari baina ya watu wanaohusika na shauri husika, kusuluhishwa bila kuwa na nia ya kutaka usuluhishi hivyo suala la usuluhishi kushindikana na kukosana kwa taasisi imara nje ya mahakama yenye ujuzi na mtaji wa kusimamia masuala ya usuluhishi.
Aidha, amesema kitendo cha baadhi ya mawakili kutokuwa tayari kuendesha mashauri kwa njia ya usuluhishi ni kutokana na maslahi binafsi ya kifedha na kukosekana kwa elimu ya usuluhishi kwa wananchi, ambapo idara ya mahakama mkoani humo imejiwekea mkakati kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kutoa elimu na kuhamasisha wadau wote wa haki kushughulikia mashauri kwa njia ya usuluhishi na kueleza faida zake kwa jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa Kigoma,Thobias Andengenye amesema kuwa utatuzi wa mashauri kwa njia ya usuluhishi ni muhimu katika kukabiliana na muda, gharama lakini kurudisha amani kwa jamii, huku akitoa wito kwa wananchi na wadau wote wanaosimamia masuala ya kupata haki kutumia fursa ya kushughulikia mashauri yao kwa njia ya usuluhishi kutokana na faida zake.
Akieleza kuhusu hali ya wananchi wa Mkoa Kigoma kupenda kumaliza mashauri yao kwa njia ya hukumu, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Mkoa Kigoma, Daniel Rumenyela amesema kuwa mashauri mengi mkoani humo yanaanzia kwenye usuluhishi lakini yanakwama na wengi kuona hukumu ndiyo njia pekee ya kupata haki zao.
Amesema kuwa, mashauri mengi yaliyopo yanahusiana na migogoro ya ardhi na kesi za madai na kwa nafasi zao wamekuwa wakijitahidi kuomba wahusika wazungumze na kumaliza kwa njia ya usuluhishi lakini inafika mahali usuluhishi unashindikana na inabaki kusubiri tafsiri ya mahakama katika kutoa haki kulingana na mwenendo wa kesi.
Comments
Post a Comment