SAKATA LA MABOMU YA MBAGALA LAWAIBUA ACT WAZALENDO
Na Mwandishi wetu, HPMedia, Dar es Salaam
Chama cha ACT Wazalendo kimeiomba Ofisi ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kulifuatilia sakata la malipo ya waathirika wa mabomu ya Mbagala na kuchukua hatua za uwajibikaji kwa watendaji walioshughulikia suala hilo kwani kuna harufu za udanganyifu, ubaguzi na uonevu.
Wito huo umetolewa leo feb 1, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kivuli wa Chama hicho, Dorothy Semu ambapo amesema watu takribani 1361 wanadai fidia zao tangu 2009 baada ya kuripuka mabomu kwenye ghala la silaha katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wanachi Tanzania( JWTZ) namba 671 KJ iliyopo Mbagala Jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa, mripuko huo umesababisha vifo, majeruhi, kuharibiwa kwa makazi na mali za watu pamoja na athari za kiafya ikiwemo magonjwa ya kifua kikuu, upofu wa macho na saratani, ambapo amebainisha kuwa wastani wa kaya 12000 ziliathiriwa na milipuko hiyo katika eneo la Mbagala pekee.
"Januari 28, 2023 nilitembelea Mbagala kufuatilia suala hili baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa waathirika hao, nilifanikiwa kufuatilia na kuchambua taarifa mbalimbali ikiwemo orodha ya waathirika, malipo, risiti za malipo, kiasi cha bajeti kilichotumika na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na baadae kutembelea baadhi ya waathirika hao"amesema Waziri kivuli Dorothy.
Aidha, amesema malalamiko mengi ya wananchi yanathibitishwa na ripoti ya CAG mwaka 2012/13 ilionyesha malipo ya fidia kwa waathirika wa mabomu ya Mbagala kulipwa kiasi cha shilingi bilioni 8 hayakuwa na nyaraka muhimu za kuthibitisha kama kweli malipo hayo yalifanyika kwa walengwa.
Hata hivyo, amesema jambo linaloumiza zaidi ni kuona viongozi wa Serikali kutoliskiliza jambo hilo kwa umakini mkubwa kwa kuwalipa stahiki zao walengwa licha ya bunge kuidhinisha bajeti ya shill billion 17, huku ikidaiwa kuwa frdha hizo zimeshatoka kwa awamu takribani sita.
Comments
Post a Comment