TMA YATOA MWELEKEO MVUA ZA MVUA ZA MASIKA
Na Mwandishi wetu, HPMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za Masika kwa kipindi cha mwezi machi hadi mei kwa mwaka 2023 ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za wastani na chini ya wastani katika maeneo mengi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TMA Dkt Ladislaus Chang’a amesema athari zinazotarajiwa kuwa ni mvua chache na zenye mtawanyiko usioridhisha katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani zinaweza kusababisha upungufu wa unyevu kwenye udongo na upatikanaji wa maji kwaajili ya shughuli za kilimo.
Amesema kuwa, mvua za msimu wa masika kwa mwaka huu ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu Kaskazini, Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Mikoa ya Pwani, mikoa ya ukanda wa ziwa Victoria na Kaskazini mkoa wa Kigoma.
"Mvua za masika zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa ziwa Victoria pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi machi 2023 na zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei 2023"amesema Dkt Chang’a.
Aidha, amesema mifumo ya hali ya hewa joto la bahari la wastani hadi juu kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la kati la bahari ya pasifiki, joto la wastani linatarajiwa katika eneo kubwa la kitropiki la bahari ya Hindi huku joto la juu ya wastani likitarajiwa katika eneo la Mashariki mwa Bahari ya Atlantiki hali hiyo itadhoofisha mifumo inayosababisha mvua.
Sambamba na hayo ametoa angalizo katika sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo na usalama wa Chakula, Mifugo na uvuvi utalii, Maliasili na wanyamapori, usafiri, Nishati, Maji na Madini, Mamlaka za miji, sekta ya afya na menejimenti za maafa kuzingatia taarifa mbalimbali za hali ya hewa na kuchukua tahadhari na kufuata ushauri wa wataalamu wa sekta husika.
Hatahivyo ametoa angalizo la uwezekano wa uwepo wa vipindi vifupi vya mvua kubwa hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Amesema mwelekeo wa mvua uliotolewa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa hivyo viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi hivyo ni vyema kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari zinazotolewa na TMA.
Hatahivyo kwa mwaka 2022 utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ulifanikiwa kwa kiwango cha asilimia 94 hivyo wataendelea kutoa mrejesho wa mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika na kuwashauri wadau kuwasiliana nao ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaja maalum katika sekta zao.
Comments
Post a Comment