Chama Cha ACT Wazalendo kimesema bajeti iliyoomba na Wizara ya Kilimo ni shilingi trilioni 1.2 sawa na asilimia 2.4 ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambayo pia haifikii kiwango kilichokubalika cha asilimia 10 ya bajeti ya Serikali kutokana na sekta hiyo kutegemewa na zaidi ya asilimia 60 ya watanzania.
Akizungumza na waandishi wa Habari Leo Jijini Dar es Salaam Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na maendeleo ya Ushirika ACT Wazalendo Mtutura Abdallah amesema wamefuatilia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo na kuifanyia uchambuzi wa kina ili kubaini kama hotuba inaakisi hali halisi ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima hapa nchini.
Amesema katika uchambuzi huo wamebaini kuwa Serikali bado haikipi kilimo kipaumbele kinachohitaji, kutokana na hoja nane walizotoa kuhusu bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwemo Mbolea ya ruzuku kutowafikia wakulima nchini.
Hoja nyingine ni Kushuka kwa bei za mazao ya wakulima nchini, Kushuka kwa uzalishaji na kasi ndogo ya ukuaji wa Sekta ya Kilimo, Uwezo mdogo wa NFRA kuhifadhi chakula jambo ambalo ni tishio kwa usalama wa nchi, Kutokamilika kwa Mradi wa ujenzi wa maghala na Vihenge vya kuhifadhia chakula, Kutofungamana kwa Kilimo na sekta ya Viwanda, Uporaji wa ardhi ya wakulima na migogoro ya wakulima na watumiaji wengine pamoja na Tishio la mazao na chakula cha GMO nchini.
Hata hivyo amesema Tanzania imeendelea kutegemea Sekta ya Kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake kwa kutoa ajira kwa asilimia 61.1 ya nguvu kazi za watanzania wote na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye miaka yenye mvua za kutosha.
Ameongeza kuwa kwa utegemezi huo mpango wa bajeti unapaswa kubeba dhima hiyo kukabiliana na changamoto za uzalishaji, uhifadhi na mauzo ya chakula Kwa kuhakikisha wakulima wanapata kwa wakati pembejeo za kilimo kwa kuwekewa ruzuku ili kuwawezesha kumudu gharama na kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha, mikakati ya kilimo lazima ifungamanishwe na viwanda ili kuongeza thamani, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha kunakuwa na masoko ya uhakika wa bidhaa za mazao ndani ya nchini na zaida kusafirishwa nje.
Sambamba na hayo amesema katika uchambuzi wao wameona Mwenendo wa bei za vyakula kuendelea kupanda ikiwa bajeti ya kilimo haitaongezwa hususani kuiwezesha NFRA kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha.
Amesema bado miradi mingi ya umwagiliaji ipo katika hatua ya ndoto, na hata iliyokwisha kuanza kutekelezwa inaenda mwendo wa mdogo hivyo kutokana na Mwenendo huu wa bajeti ya kilimo itachukua muda mrefu zaidi kupiga hatua ya maana nchini.
Comments
Post a Comment