TBC NA VON WAINGIA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KATIKA NYANJA ZA HABARI


Na Mwandishi wetu  HabariPlus 

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) leo limeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Sauti ya Nigeria (VON) katika nyanja tano za habari  kwa lengo kukuza lugha ya kiswahili na mahusiano mazuri yaliopo baina ya nchi hizo mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt Ayub Rioba Chacha amesema kuwa pamoja na mambo mengine mashirikiano hayo watabadilishana maudhui ya vipindi na matangazo mbalimbali.

Amesema kuwa, kupitia mashirikiano hayo Tbc itakwenda kuisaidia idhaa ya kiswahili ya Von kupata watangazaji wa kiswahili, wataalamu wa kufundisha kiswahili na kutoa mafunzo mengine ya lugha hiyo.

Ameongeza pia watakwenda kushirikiana katika kubadilishana wafanyakazi kutoka nyanja za habari, utangazaji, ufundi wa mitambo ambapo Tbc tayari imeshapeleka mtangazaji wake mmoja Von ili kusaidia katika matangazo ya kiswahili.

"Tutashirikiana katika kutoa fursa za kuwezesha kupata au kuweka wawakilishi wa vyombo vya habari katika nchi husika, yaani Tbc itakua na mwakilishi Nigeria na Von itakua na mwakilishi wake Tanzania "amesema Dkt Rioba.

Aidha amesema, katika kuhakikisha ushirikiano huo unadumu kati ya Tanzania na Nigeria, darasa la kiswahili limeanzishwa nchini Nigeria ili wawekezaji wa nchi hiyo waweze kutumia kutumia lugha hiyo wanapotembelea Afrika Mashariki.

Ameongeza kuwa, kumekua na mazungumzo ya kushirikiana mafunzo ya lugha ya kiswahili na chuo kikuu cha Port Harcourt, pia chuo kikuu cha Ghana kinatoa mafunzo ya shahada ya lugha ya kiswahili.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa VON Jibrin Baba Ndace amesema kuwa mashirikiano hayo yatasaidia kukuza ajenda ya Afrika kutokana na umuhimu ulioonekana kwa waafrika wenyewe kueleza masuala yanayowahusu kwa mtazamo wa Afrika.

Makubaliano yaliosainiwa leo yana historia toka enzi za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kupitia idhaa ya kiingereza ambapo ilikua na ushirikiano wa karibu na shirika la utangazaji la Nigeria (NBC) kupitia idhaa ya matangazo ya nje ambayo yalihanikiza shughuli za ukombozi wa Afrika.

Hata hivyo,baada ya bara zima kupata uhuru ushirikiano huo ulififia kutokana na mabadiliko yaliotokea katika mfumo wa kisiasa na kiuchumi duniani kudhoofisha umajui wa Afrika na nchi husika kuanza utegemezi katika nyanja mbalimbali kutoka mataifa ya nje hususani Ulaya na Marekani.



Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI