SEKTA YA KILIMO KUNUFAIKA NA MRADI WA KUTENGENEZA MBOLEA WA SHILL TRILL 3.2
Na mwandishi wetu, Habari Plus
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Uwekezaji imesema itaendelea kuboresha mazingira rafiki na wezesheji kwa wawekezaji ambapo katika kuendelea kuboresha Sekta ya kilimo Groundbreaking Venture Tanzania imesaini Mradi wa kutengeneza Mbolea wenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.2.
Mkataba huo wa Makubaliano (MOU) ni kati ya ESSA Industries kutoka Indonesia na wadau wa Tanzania TIC, TFRA, na TPDC ukilenga kuleta Mapinduzi kwenye sekta ya Kilimo ambapo pamoja na mambo mengine umelenga kuzalisha ajira na kutatua changamo ya upatikanaji wa mbolea.
Hafla hiyo ya utiaji saini imeshuhudiwa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, ambapo amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza tija katika sekta ya kilimo hapa nchini.
Aidha amesema kuwa MOU hiyo ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa Tanzania kwenye sekta ya kilimo, kuhakikisha usalama wa chakula, na kukuza uchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo amesema kuwa mradi huo ni muhimu sana kwa Tanzania kwani wanategemea mbolea asilimia 90 kutoka nje ya nchi na asilimia 10 ndio wanazozalisha wao hivyo mradi huo utasaidia sana katika uzalishaji.
"Mradi huu utatusogeza kwa miaka 3 hadi mitano ijayo, hakuna mapinduzi ya viwanda bila kilimo, tunahitaji mbegu bora, udongo mzuri, ambapo hatua hii inahitaji umwagiliaji, namna pekee ya kuondoa changamoto za ajira ni kuendeleza kwenye viwanda na kuongeza kasi kwenye uzalishaji"amesema Waziri Prof Kitila.
Naye, Kamishna wa Sekta ya ESSA, Rahul Puri ameieleza kuwa thamani ya Mradi huo ni Dola 1.2 bilioni sawa na Shilingi trilioni 3.2 za kitanzania ambapo inatarajiwa kuzalishaji tani milioni 1 za mbolea kila mwaka.
Ameongeza kuwa mradi huo utaweza kuzalisha ajira 389,000 na Matumizi ya gesi futi za ujazo milioni 70 kwa siku (mmcfd).
Hata hivyo amesema wanaotarajia mradi huo kufikia mwaka 2025 kukamilisha kandarasi ya gesi ili kuwezesha uzalishaji wa tani milioni 1 za urea kila mwaka na kufikia 2029 mradi unatarajiwa kufanya kazi kikamilifu.
Mradi huo ni matokeo ya moja kwa moja ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan mwezi Januari nchini Indonesia, akisisitiza dhamira ya mataifa yote mawili kuimarisha uhusiano wao wa kibiashara na uwekezaji.
Comments
Post a Comment