HESLB, NIDA KUFANYA KAZI PAMOJA,ZATOA WITO KWA WANAFUNZI
Imeelezwa kuwa upatikanaji wa namba ya utambulisho (NIN) kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni hitaji la lazima hasa wale wanaoomba mikopo kwa mwaka wa masomo 2025/26.
Aidha, upatikanaji wa namba za utambulisho kwa wanafunzi watakaoomba mikopo utasaidia kupatikana kwa taarifa sahihi na muhimu kwa muombaji wa mkopo huo.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu( HESLB) na Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa( NIDA)zimekubaliana kutumia namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) kwa ajili ya kupata taarifa sahihi za wanafunzi wanao omba kuanzia mwaka huu wa masomo 2025/2026.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia amesema kwamba kuanzia mwaka huu mpya wa masomo 2025/2026 namba ya Utambulisho itakua ni hitaji la lazima la kila muombaji mkopo atakae enda kuomba kupitia mifumo yetu ya Bodi hiyo.
Aidha Dkt.Kiwa amewashauri waombaji wote wa mikopo kuhakikisha wanapata namba za utambulisho mapema iwezekanavyo kabla ya dirisha la maombi halijafunguliwa na ndani ya muda wa maombi ya mkopo kabla ya dirisha la maombi halijafungwa.
"Hii namba ya Utambulisho( NIN)napenda kuutaarifu umma kwamba taasisi zetu hizi mbili(HESLB na NIDA)zimechukua hatua muhimu sana za kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa ufanisi nakwa wakati,tayari tumeshaunganisha mifumo yetu inasomana "amesema Dkt. Kiwia.
Ameongeza" Tumeamua kutumia namba ya Utambulisho( NIN) kwasababu ni namba ya utambulisho wa uhakika unaosaidia kupata uhalali wa taarifa za muombaji wa mkopo,pia itasaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Bodi yetu kutokana na kupata taarifa za uhakika naza kipekee za kila mwanafunzi"
Amesema kwamba HESLB ina majukumu ya kutoa mikopo na kukusanya mikopo, hivyo kwa kutumia namba ya utambulisho(NIN) itaweza kuboresha uwezo wa kufuatilia nakuwapata wanufaika waliokopeshwa baada ya kuhitimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa( NIDA) James Kaji amesema dhamira ya Serikali kwa ujumla ni kuona kila mwanafunzi aliyemaliza elimu ya Sekondari mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea na raia wa Tanzania, anasajiliwa na kupata Namba ya Utambulisho( NIN) na kitambulisho cha Taifa itakayomwezesha kujiunga na masomo ya ngazi za juu na kati pamoja na kuomba mkopo wa masomo.
Aidha, Kaji ameihakikishia Bodi ya Mikopo kuwa NIDA imejipanga kikamilifu kutoa huduma bora zaidi na kuendelea kushirikiana kwa karibu na HESLB ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma za usajili kwa wakati ili waweze kufanikisha upatikanaji wa mikopo yao.
"Tunapofanya majukumu yetu yaliyo upande wetu,niwaombe wanafunzi kwa upande wao nao watekeleze wajibu wao,kwa kuchukua hatua ya kujisajili mapema,msisubiri matukio kama hayo niliyoyataja ya kudahiliwa vyuoni au ajira ndipo mjitokeze ambapo muda unakuwa hautoshi lakini pia kuwafanya watumishi wa NIDA kuzidiwa kwa kuwa mnakuwa wengi kwa wakati mmoja" amesisitiza MD Kaji.
Comments
Post a Comment