WAZIRI MAVUNDE KUZINDUA KAMATI YA TAMISA


Na Mwandishi wetu 

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde anatarajiwa kuzindua Kamati ya Chama cha Wasambazaji wa Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), ambapo uzinduzi huo utaambatana na kufanyika kwa kongamano la kuwaunganisha watanzania waliopo katika sekta ya madini.

Aidha, wafanyabiashara wazawa,wadau katika sekta ya madini na chama cha wachimbaji wadogo wa madini wametakiwa kujiunga na taasisi ya usambazaji sekta ya madini Tanzania (TAMISA) kwa lengo la kuwa na sauti moja katika kuzifikia fursa zilizoko.

Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISA, Masoko na Mawasiliano, Dk. Sebastian Ndege katika mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa pia na Mwenyekiti wa TAMISA Peter Kumalilwa.

Amesema kwamba uzinduzi huo utafanyika 16/5/2025 Jijini Dar es Salaam utakuwa na matukio mawili, la kwanza ni kuzindua Kamati ya TAMISA na tukio la pili litakuwa ni Kongamano ambalo litazungumzia nafasi ya Watanzania katika utoaji huduma kwenye sekta ya madini.

"Tunafahamu sisi watanzani madini ni ya kwetu, na tunafahamu ya kuwa tunakila sababu ya kushiriki katika uchumi wa madini na Serikali yetu pamoja na Waziri wetu Mavunde amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika sekta hii," amesema Dkt. Ndege.



Kwa upande wake Mwenyekiti TAMISA, Kumalilwa amesema Waziri Mavunde amekuwa akiongelea kuwa katika sekta hii ya madini kuna kiasi cha shilingi trilioni 3.1 ambayo inatumika kila mwaka katika manunuzi ambayo angependa Watanzania wanufaike nayo.

"Kuna migodi mikubwa nchini kama mitano, ambayo wao kila mwaka wanafanya manunuzi ya shilingi trilioni 3.1, ambapo sisi watanzania tunanufaika kwa karibu asilimia 10 tu, kiasi hiki ni kidogo sana" amesema Kumalilwa.

Amesema kwa kutambua hilo TAMISA imeweka mikakati ya kuhakikisha watanzania zaidi wanaanzisha viwanda vya madini na kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo ili kuweza kunufaika japo na asilimia 30 ya kiasi cha hicho shilingi trilioni 3.1 za manunuzi ya sekta ya madini.

"Kwa sasa hivi sisi Tanzania tunasheria ya local content, kwa wakati wangu kama Mkwenyekiti wa TAMISA nitahakikisha Watanzania wananufaika na shilingi trilioni 3.1 za manunuzi japo kwa asilimia 20 hadi 30," amesema Kumalilwa na kuongeza,

"Tumekuwa tukilalamika sana kuhusu Wachina wanakuja nchini wanachukua kazi zetu, sasa sisi kama TAMISA tumekuwa tukihakikisha kwamba tunawajengea uwezo Watanzania ili waweze kushiriki katika uchumi wa sekta ya madini nchini,"amesema Kumalilwa.

Aidha, ameongeza kuwa TAMISA, itakua na majukumu kadhaa ikiwemo kuhamasisha wazawa kujiunga na vyama vya madini, kuhabarisha wadau hususani wazawa fursa zinazopatikana kupitia sekta hiyo sanjari na kuwaunganisha wadau wazawa kuwa na sauti moja na kufikia mafanikio yanayohitajika.

TAMISA iliyozinduliwa Septemba 15, 2024 na Waziri wa Madini,  Anthony Mavunde, inamalengo makuu ya kutetea wasambazaji wa sekta ya madini, kuboresha uwezeshaji wa biashara, kutetea haki za wasambazaji na kuendeleza utafiti na ukuaji wa teknolojia.



Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI