OFISI YA MSAJILI WA HAZINA, JULAI 2024/MEI 2025 YAKUSANYA SH BILL 884.7, LENGO KUFUKIA TRILL 1
Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema Serikali imekusanya shilingi bilioni 884.7 kwa kipindi cha miezi 11 yaani kuanzia Julai 2024 hadi Mei 2025 ikiwa ni makusanyo ya mapato yasio ya kodi huku ikiwa na shauku ya kukusanya shilingi trilioni 1 katika mwaka huu wa fedha wa 2024/25.
Aidha ongezeko hilo ni kubwa la mapato yanayokusanywa kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, ikilinganishwa na Sh bill 633.3 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2023/24.
Akizungumza katika kiko na wahariri na waandishi wa habari wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu ameeleza kuwa hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 40, ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita.
Ameseam kupitia ongezeko hilo inaonyesha ongezeko la asilimia 15.3 ikilinganishwa na jumla ya makusanyo ya mwaka mzima ya Shilingi bilioni 767 katika mwaka wa fedha uliopita.
Mchechu amesema ukuaji huo wa mapato umetokana na kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika Mashirika ya umma na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.
"Ofisi imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Mpango na Bajeti (PlanRep) na Mifumo ya ERMS na e-Watumishi pamoja na kufanya maboresho ya Mfumo wa MUSE ambao unawezesha kupata taarifa halisi za matumizi katika Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za Umma,"amesema Mchechu
Amesema maboresho hayo sasa yamefanya mifumo kubadilishana taarifa ipasavyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuona mifumo inasomana.
Akivitaja vyanzo vikuu vya mapato kwa mwaka huu amesema ni gawio ambalo limechangia asilimia 63.9 ya mapato yote, huku michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ikichangia asilimia 29.7.
Aidha, amesema mapato mengineyo yaliyojumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) yamechangia asilimia 6.4 ya mapato yote.
Ameongeza vyanzo vingine ni makusanyo ya mapato, pia uwekezaji katika kuimarisha utendaji wa watumishi wao kupitia viashiria muhimu vya utendaji (KPIs) umetajwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyofanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
"Kupitia KPIs, Ofisi hiyo imeweza kufanya tathmini za utendaji wa Bodi, ili taasisi ziwe na matokeo yanayopimika kwa uwazi na uwajibikaji. Hili limeenda sambamba na kuwajengea uwezo Viongozi wetu ambapo jumla ya Watendaji Wakuu 111 walishiriki mafunzo elekezi ya uongozi na usimamizi (CEO Induction) mwaka huu, ili kuimarisha utawala bora na uhusiano wa kiutendaji,” alisema Mchechu.
Hata hivyo, amesema ili kuongeza ufanisi zaidi na ukusanyaji wa mapato, Serikali iliongeza uwekezaji wake katika mashirika ya umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
"Sasa thamani ya uwekezaji wake imetoka Sh75.79 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh86.29 trilion imwaka 2023/24. Pia tumeweza kuhamasisha uwajibikaji katika kampuni hizi kupitia Mkutano wa Wakurugenzi wa Bodi wanaoiwakilisha Serikali katika kampuni zenye hisa chache uliowaleta washiriki 125 na kuzindua Mwongozo Ulioboreshwa wa Wakurugenzi,"amesema Mchechu.
Kwamba hilo, limeenda sambamba na kupitia Mikataba na Kuimarisha Usimamizi wa Hisa huku ikiongeza ushiriki wake katika kampuni muhimu kwenye sekta za benki, viwanda na madini kupitia maboresho ya mikataba ya wanahisa na miundo ya usimamizi.
Akizungumza kuhusu Siku ya Gawio (Gawio Day), Mchechu amesema siku hiyo ya Gawio inatarajiwa kufanyika Juni 10, mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam ma kwamba katika siku hiyo, taasisi na mashirika ya umma yatamkabidhi rasmi Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan, michango na gawio kwa Serikali.
"Tukio hili ni muhimu sana si tu kama alama ya uwajibikaji, bali pia kama chombo cha kutathmini utendaji wa mashirika na taasisi za umma kwa mujibu wa malengo ya Taifa," ameeleza Mchechu.
Amesema Siku ya Gawio imekuwa kichocheo kikubwa cha mageuzi na mafanikio yanayooneka leo kwani tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu wa wazi na wenye uwajibikaji, kumekuwa na ongezeko la mashirika yanayotoa gawio, pamoja na kuboreshwa kwa utendaji wao kwa ujumla.
"Hii ni ishara kuwa pale ambapo taasisi za umma zinasimamiwa kwa weledi, mafanikio ya kweli yanawezekana,” amebainisha Mchechu.
Comments
Post a Comment