ABIRIA WA MASAFA MAREFU WAPEWA USHAURI HUU NA LATRA CCC
Na Fatma Ally
ABIRIA wanaosafiri masafa marefu wametakiwa kuwa makini pindi wanapokata tiketi kwa kuzikagua vizuri na kujiridhisha kama zinataarifa zao sahihi ili kuepuka usumbufu pindi inapotokea hitilafu wanapokua njiani.
Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (Latra CCC) Daud Daud wakati alipokua kwenye maonyesho ya 49 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere (Sabasaba).
Amesema kuwa, kukosekana kwa taarifa sahihi za abiria kwenye tiketi imekua changamoto kubwa inayowakabili wasafiri wengi kwani endapo likitokea tatizo, chombo kimepata hitilafu ikabidi abiria wahamishwe kutoka chombo kimoja kwenda kingine,lazima gari itakayowapokea akague tiketi zao.
"Abiria wengi wamepatwa na changamoto hiyo,mtu anakuambia mimi ofisini waliniambia gari hii inafika labda Kilombero,tumefika Msamvu wanasema ndo mwisho wa safari,sisi kama baraza la ushauri tunapopokea changamoto kama hiyo inatuwia ngumu sana kumsaidia kwasababu ili tumsaidie lazima tuwe na nyaraka za kurejea na waraka wa kusafiria hua ni tiketi,tukikuta tiketi inasema Dar es salaam-Msamvu lakini yeye anenda Kilombero inabidi kutumia busara kumsaidia".amesema Daud.
Amesema kuwa, wamefika katika maonyesho hayo lengo ni kutoa elimu kwa jamii kwani wanakutana na watu wengi wanapata fursa ya kutoa maoni yao au changamoto wanazokumbana nazo wanapokua safarini na sio Dar es Salaam peke yake bali kwa nchi nzima.
"Tumepokea malalamiko mengi kwani hapa wanakuja watu kutoka mikoa tofauti tofauti sio Dar peke yake tumekuwa tukiwambia haki zao na wajibu wao kabla hujasafiri tafuta taarifa sahihi,hakikisha unafanya malipo sahihi ili uweze kupata tiketi ambayo ni halali,inayosomeka majina yako sahihi na pia ionyeshe unatoka wapi na unaenda wapi"amesema
Amesema kuwa, abiria wengi pia wamekua wakilalamikia changamoto ya kupata muda mdogo wa mampuziko wanapokua safarini jambo ambalo si sahihi kwani walitakiwa kutumia muda wa dakika 30 kupata chakula kwani wanakua wamechoka sana kutokana na umbali wa safari.
Akizungumzia changamoto za masafa mafupi (Daladala) amesema pia wamepokea malalamiko ya abiria kukatishiwa ruti na wakati mwengine kupandiahiwa nauli kiholela wanapokua vituoni kutoka 700 hadi 1000.
"Mtu amepanda gari ambayo inaitwa Kariakoo -Gongolamboto lakini ikifika Ukonga abiria wakashuka wengi, akawaona tena abiria wengi wanataka kurudi mjini anageuka,ambapo mara nyingi hii wanaifanya muda ambao abiria ni wengi, hiyo ni changamoto kubwa kwani sio kwa daladala za Dar es salaam tu bali kwa mikoa yote"
Aidha, amesema kutokana na maoni waliyoyapokea Baraza hilo, wanayachukua na kuyaweka kwenye ripoti yao kwa ajili ya kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kila mmoja anawajibika katika nafasi yake na kuhakikisha abiria wanapata haki zao.
Comments
Post a Comment