INEC KUSHIRIKIANA NA VYOMBO VYA HABARI UCHAGUZI MKUU 2025


Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeahidi kutoa ushirikiano wa karibu kwa vyombo vya habari nchini katika kuhakikisha taarifa za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 zinapatikana kwa wakati na kwa usahihi.

Akifungua mafunzo ya Wahariri na Waandishi wa Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika ukumbi wa Mlimani City leo tarehe 4 Agosti 2025, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu Kailima R.K., amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi, Tume itashirikiana na waandishi wa habari kupitia njia mbalimbali ikiwemo kushiriki katika vipindi vya redio na televisheni, pamoja na kutoa taarifa rasmi kwa wakati unaofaa ili kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa habari za kweli na zisizo na upotoshaji.

“Tunaamini kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa amani. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha habari zinazotolewa zinazingatia maadili ya uandishi wa habari na kuepuka maudhui yanayoweza kuchochea chuki au ghasia,” amesema Ndugu Kailima.

Mkurugenzi wa Uchaguzi amesisitiza kuwa Tume itatoa taarifa sahihi na kwa wakati, na itatoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kila wanapohitaji ufafanuzi au msaada wowote wa kihabari.

Aidha, Ndugu Kailima ameeleza kuwa Tume itazindua mfumo wa kusajili vyombo vya habari kuanzia tarehe 1 hadi 30 Septemba 2025.

“Mfumo huu utasaidia vyombo vya habari kupata vibali na vitambulisho rasmi vya waandishi wake kwa ajili ya kufanikisha kazi zao wakati wa Uchaguzi Mkuu,” ameeleza.

Kufanyika kwa mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kumehitimisha mfululizo wa mikutano ya wadau ambayo ilianza tangu tarehe 27 Julai 2025, ambapo Tume ilikutana na viongozi wa vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali,

wawakilishi wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na watayarishaji wa maudhui ya mtandaoni.

Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI