NLD YAZINDUA ILANI YA UCHAGUZI
Na Mwandishi wetu
Chama cha National League for Democracy (NLD) limezindua ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Ilani hii imewasilishwa kwa umma na uongozi wa chama ikiwa ni dira na mwelekeo wa kisera kwa mgombea urais kupitia tiketi ya NLD, Doyo Hassan Doyo, kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kuwaongoza Watanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo Cha Mawasiliano imeeleza Ilani ya NLD imejengwa juu ya misingi ya Uzalendo, Haki na Maendeleo, na imejikita katika vipaumbele vinne vikuu vinavyolenga kuleta mabadiliko ya kweli na maendeleo jumuishi kwa kila Mtanzania
NLD inatambua changamoto ya ukosefu wa ajira, hususan miongoni mwa vijana. Kupitia ilani hii, chama kinapendekeza mikakati ya kuanzisha viwanda vidogo na vya kati, kuimarisha sekta ya kilimo cha kisasa, pamoja na kuwezesha vijana na wanawake kupitia mikopo, mafunzo, na ujasiriamali.
Aidha, Lengo ni kupunguza utegemezi, kuongeza uzalishaji wa kitaifa, na kukuza uchumi wa wananchi mmoja mmoja.
NLD inaamini kuwa elimu ni nguzo ya ustawi wa taifa. Ilani ya chama inalenga kuhakikisha elimu bora, inayopatikana kwa wote bila ubaguzi wa kiuchumi au kijamii, huku mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji yakiimarishwa, pamoja na maslahi ya walimu kupewa kipaumbele.
Lengo. Kujenga kizazi chenye maarifa, ujuzi na maadili kwa ajili ya mustakabali wa taifa.
Ilani ya NLD inalenga kuimarisha huduma za afya kwa kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, miundombinu ya afya, pamoja na kupanua wigo wa bima ya afya kwa wananchi wote wakiwemo wa kipato cha chini.
Lengo. Kujenga jamii yenye afya njema, yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Miundombinu bora ni kichocheo cha maendeleo ya taifa. NLD imejipanga kuwekeza katika barabara, reli, nishati, na teknolojia ya mawasiliano kwa lengo la kuunganisha Watanzania, kupunguza gharama za uzalishaji, na kuongeza ushindani wa taifa katika soko la kikanda na kimataifa.
Kupitia Ilani hii, Chama cha NLD kinaweka mbele matumaini ya Watanzania kwa kutangaza ajenda ya mabadiliko ya kweli, yanayolenga watu, uchumi, na ustawi wa taifa.
Kwa msingi huo, NLD kinawaomba Watanzania wote kuungana na kuunga mkono mwelekeo mpya wa Taifa, kwa kumpa Mhe. Doyo Hassan Doyo ridhaa ya kuwaongoza katika kulijenga taifa lenye Uzalendo, Haki, na Maendeleo kama sehemu ya kuleta usawa na fursa kwa Watanzania wote.
Comments
Post a Comment