TANESCO YAJA NA MATUMAINI TELE KWA WANANCHI
Na mwandishi wetu HPMedia, Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme nchini unakuwa wa kudumu, Shirika la Umeme nchini TANESCO linaendelea na ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ambalo limefikia asilimia 80.22 hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2022.
Aidha, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema kwa sasa hali ya upungufu wa umeme nchini umepungua kwa kiasi kikubwa na kufanya hali ya upatikanaji wa umeme kuboreka zaidi hivyo kupunguza adha ya mgao wa umeme uliokuwepo hapo awali.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Maharage Chande amesema maboresho ya upatikanaji wa umeme yametokana na mipango ya muda mfupi na wakati ambayo imekwishatekelezwa na shirika hilo pamoja na uwepo wa mvua za vuli.
Amesema kuwa, urefu wa kina cha maji la bwawa hilo umefikia mita 126.12 kutoka usawa wa bahari na bado wanaendelea kujaza maji na linatarajiwa kujaa baada ya misimu minne ya mvua za vuli na masika na wataanzisha miradi ya vituo vipya vya kutumia gesi na umeme jadidifu.
Aidha amesema kuwa katika mipango ya muda mfupi tayari wameshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kinyerezi namba II na umeshaanza kuzalisha megawati 45 za umeme kwenye Gridi ya Taifa kuanzia Novemba 24 /2022 pamoja na mitambo miwili iliyopo katika kituo cha Ubungo namba III.
Hata hivyo, amesema kuwa tayari wameshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha kidatu na unazalisha megawati 50 za umeme kwenye Gridi ya Taifa pamoja na ufungaji wa mitambo mitatu iliyopo katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I na kinaingiza megawati 120 za umeme kwenye Gridi ya Taifa.
Amesema kuwa, licha ya upatikanaji umeme kuboreka shirika linaendelea kushuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya umeme kutoka asilimia 6 hadi 11 kwa mwaka ambapo ongezeko hilo limeshuhudiwa kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, amesema kuwa mvua za vuli zilizonyesha hivi karibuni hazikuwa toshelevu kama ilivyotegemewa hivyo shirika bado litaendelea kufanya matengenezo ya mitambo yake ambayo haikufanyiwa matengenezo kwa muda mrefu na watatoa taarifa kwa wateja pindi yatakapofanyika.
Comments
Post a Comment