AZAM TV KUPOKEA FILAMU ZENYE VIWANGO VYA KIMATAIFA, YAZINDUA FILAMU MBILI



Na fatma Ally,  HPMedia, Dar 

Mkuu wa Chaneli ya Sinema zetu Sophia Mgaza amesema wanatarajia kuanza kupokea filamu hivi karibuni ambazo wanategemea kupata hadithi zenye utafiti wakutosha, uhalisia wa kitanzania na kugusa jamii na hadithi zenye stori ndefu isiyopungua dakika 90 na yenye viwango vya juu vya kimataifa inayoweza kuchezwa kwenye majumba ya Sinema pamoja na bajeti yake.

Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam alipokua akizungumza na waandishi wa habari, wakati  Kampuni ya Azam TV kupitia chaneli yake ya Sinema zetu ilipokua ikizindua tamthilia mbili za moto ambazo ni Lolita na Mtaa wa Kaza moyo ambazo zinatarajiwa kuruka kuanzia tarehe 4 na 14 mwezi wa August mwaka huu chaneli 103.

Aidha amesema tamthilia hizo zilizobeba simulizi za kuvutia si tu kwamba zinakuja kuleta mapinduzi ya tasnia ya tamthilia nchini, bali zinaakisi maisha halisi ya Watanzania wa rika zote na zinahusisha waigizaji wenye vipaji na viwango vya juu.

“Uzalishaji wa tamthilia hizi mbili Mtaa wa Kazamoyo na Lolita umezingatia mahitaji ya soko kwani umetumia vifaa vya uzalishaji vya kisasa na ubora wa hali ya juu wenye uwezo wa kutoa kazi katika viwango vya picha zenye ubora na angavu yaani HD (High Definition). Lengo letu la kufanya mambo yote haya ni kuendeleza dhamira yetu ya kutoa burudani ya hali ya juu kwa watazamaji wetu"mesema Mgaza.

Akizungumzia kuhusu tamthilia ya Mtaa wa Kazamoyo Muandaaji wake Mahsein Awadhi (Dkt. Cheni) amesema tamthilia hiyo inasimulia hadithi inayohusu maisha ya uswahilini na matukio wanayopitia wakazi wa Mtaa wa Kazamoyo, huo ni mtaa wenye sifa ya wanawake kukaa vibarazani na kupiga stori, porojo pamoja na umbea huku vijana wa mtaa huu wakichagua maisha ya kuwa vibaka ili kupata vipato kwa njia fupi na nyepesi kwao.

Kwa upande wake, Muandaaji wa Tamthilia ya Lolita, William Mtitu amesema tamthilia hiyo inatoa simulizi ya maisha ya vijana wa kisasa na namna wanavyokabiliana na changamoto za kimahusiano yaliyojaa usaliti. Tamthilia hii pia inatoa simulizi ya familia mbili zilizodhulumiana pesa na hivyo kila upande ukiapa kulipiza kisasi kwa mwenzake.

Hata hivyo tamthilia hizo zinachukua nafasi ya Fungu Langu itakayofikia tamati tarehe 29 Julai 2023 na Jeraha itakayofikia tamati tarehe 10 Agosti, 2023 ambapo Burudani zote hizo zinapatikana kwa malipo ya kifurushi cha Shilingi 8,000 kwa watumiaji wa kisimbuzi cha dishi na antena.

Comments

Popular posts from this blog

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

HUU HAPA MWENENDO WA KIMBUNGA "HIDAYA" , UPEPO KUVUMA KWA KASI YA KILOMITA 130 KWA SAA

NHIF YAFANYA MABORESHO YA KITITA CHA HUDUMA ZA MATIBABU, YAENDELEA KUPOKEA MAONI