PODIUM INC KUWANOA WAANDISHINWA HABARI
Na Mwandishi wetu HPMedia, Dar
Katika kukuza sekta ya habari hapa nchini Kampuni ya Podium inayojihusisha na masuala ya Habari, Mawasiliano na Utafiti imeandaa mijadala ya kila mwezi ambayo inatarajiwa kuanza mwisho wa mwezi wa nane na itahusisha wanahabari hususani vijana wanaochipukia ili kuhakikisha kuwa jamii inapata taarifa kwa usahihi.
Haya yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Podium Ezekiel Kamwaga ambapo amesema kupitia mijadala hiyo wanahabari watapewa fursa ya kujifunza jinsi ya kuripoti taarifa mbalimbali za kimataifa na kujiongezea maarifa kwa mambo ambayo hawakufundishwa vyuoni.
“Kupitia mijadala hiyo wanahabari watatuambia wao wanataka mafunzo gani pengine vyuoni hayakuwepo ila wameingia kazini wakakutana nayo, hivyo nitakuwa namleta mtu kufundisha kile ambacho wanataka kufundishwa, pia nitatoa elimu kuhusu matukio makubwa yanayotokea Duniani kama Tanzania tunakipi cha kujifunza mfano kwa sasa Mapinduzi yaliyotokea katika nchi ya Niger kutokana na mafunzo niliyopata Uingereza kuhusu Siasa za Afrika nami niwashirikishe wengine” Amesema Bw. Kamwaga.
Aidha amesema lengo la Podium ni kusaidia watu kutoka sehemu walipo na kuwapeleka hatua nyingine ikiwemo mashirika mbalimbali, wanahabari na watu binafsi.
Sambamba na hayo amesema mbali na mijadala hiyo pia wana gazeti la Dunia la mtandaoni ambalo linachambua habari za kisiasa kwa viwango vya kimataifa kwa lugha ya Kiswahili.
“Mimi nafahamu lugha ya kingereza na kifaransa, uchambuzi unaofanywa kwenye gazeti la Dunia ni wa viwango vya juu kuliko hata kwenye vyombo vingine vya kimataifa, mfano chambuzi anazozifanya mwandishi mkongwe Ahmed Rajab kwenye gazeti la Dunia zina ubora zaidi kuliko zile zinazoandikwa na mashirika mengine ya kimataifa na anaandika kwa viwango vya kimataifa na kwa lugha ya Kiswahili ambayo kwa sasa inawazungumzajj zaidi ya milioni 200"Ameongeza Bw. Kamwaga.
Hata hivyo ametoa wito kwa waandishi wakongwe kutambua kuwa wanawajibu wa kuwasaidia waandishi wanaochipukia na hawana bahati ya mafunzo kama walivyopata wao kutoka kwa waandishi wenye uzoefu waliokutana nao.
Katika hatua nyingine amesema ukiaji wa teknolojia ni fursa kwa waandishi wa habari kwani takribani asilimia 70 ya Watanzania ni vijana ambao taarifa nyingi wanazifuatilia mitandaoni hivyo waitumie vizuri kuhakikisha kuwa watu wote wanapata taarifa sawa wa mjini na vijijini.
Ameongeza kuwa wanahabari wanaochipukia mitandao ndio sehemu yao ya kujidai hivyo wanachopaswa kupewa ni uelewa, maarifa ili ajue jinsi ya kutoa taarifa kwa jamii ili kupunguza kiwango cha uwepo wa habari ambazo hazijaandikwa vizuri na hatarishi kwa umma.
Ametoa wito kwa wanahabari kutokata tamaa licha ya changamoto iliyojitokeza kipindi cha miaka 15 iliyopita ya kupungua kwa vyombo vya habari kwani hali sasa inarudi, kujiongeza kwa kufanya vipindi vya kibunifu na kuongeza maarifa.
Kampuni y Podium mbali na kujihusisha na masuala ya Habari pia inafanya kazi ya mahusiano na jamii, kampuni, vyama vya siasa na Asasi za kiraia toka nje ya nchi pia kufanya tafiti kwa kampuni zinazotaka kuwekeza sehemu mbalimbali hapa nchini na hazina uelewa wakutosha kuhusu njia gani au taarifa zipi ambazo watanzania wanapendelea na ambazo zitawaletea tija kwenye uwekezaji wao.
Comments
Post a Comment