WANAOPANDISHA BEI YA SUKARI KIHOLELA KUKIONA


Na Mwandishi wetu, Dar

KATIKA kukabiliana na uhaba wa sukari nchini Tanzania Serikali imetoa kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi tani 50,000 ambapo inatarajiwa kuingia Januari 22, mwaka huu pamoja na kuvifungulia viwanda vyote vinavyozalisha sukari  ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania Prof Kenneth Bengesi wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema sukari iliyopo nchini kwa sasa haikidhi mahitaji ya wananchi, hivyo Serikali imejipanga kuchukua hatua ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Amesema kuwa, miongoni mwa sababu zilizopelekea kuwepo kwa changamoto hiyo ni pamoja na mvua za El-nino ambazo zimenyesha mwezi Novemba na Disemba mwaka 2023 ambapo zimesababisha mashamba ya miwa kujaa maji na miundombinu hivyo kupelekea uzalishaji mdogo wa miwa.

Katika hatua nyengine Bodi ya Sukari Tanzania imewataka wafanyabiashara wanaouza sukari kuacha tabia ya kujipangia bei hali  inayopelekea kuwaumiza wananchi kwani bei ya sukari kwa sasa wanauza hadi shill 6000 kutoka 3000 bei ya kawaida.

"Tumeshangazwa na taarifa tunazozisikia kuwa huko mtaani bei ya sukari imepanda sana, hakuna bei mpya ambayo imetoka wananunua kwa bei ile ile, sijui kwa nini wanapandisha, Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha inatatua tatizo hili, hawa wanaojipangia bei tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria"amesema Prof Kenneth.

Ameongeza kuwa, "Bodi inatambua kuwa kila mkoa unatofautiana bei ya sukari hivyo wafanyabiashara wanaopandisha bei kwa maslahi yao binafsi tofafauti na bei halali ya mkoa huo tukiwabaini hatutawaacha tutahakikisha tunawachukulia hatua kali za kisheria kwani hatupendi kuona wananchi wakilalamika juu ya bidhaa hii muhimu kupandishiwa bei holela” amesisitiza mkurugenzi.

"Mwaka 2023 tumezalisha tani 345,000 pekee ambazo hazitoshelezi lakini kawaida mahitaji huwa ni tani 520,000 na katika uzalishaji tunapenda malengo yetu ni kuzalisha tani laki tano na hamsini na tano ili tuwe na akiba ya sukari ya kutosha lakini kutokana Msimu huu wa mvua za El nino tumeshindwa kufikia lengo ndiyo maaana tuna uhaba wa sukari"amesema Bengesi.

Comments

Popular posts from this blog

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

HUU HAPA MWENENDO WA KIMBUNGA "HIDAYA" , UPEPO KUVUMA KWA KASI YA KILOMITA 130 KWA SAA

NHIF YAFANYA MABORESHO YA KITITA CHA HUDUMA ZA MATIBABU, YAENDELEA KUPOKEA MAONI