WANANCHI RUFIJI WAISHUKURU TAWA KWA KUWAOKOA DHIDI YA ATHARI ZA KUCHEPUKA KWA MTO

Na. Beatus Maganja 

Wananchi wa Kijiji cha Ngarambe, Kata ya Ngarambe wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani wameishukuru Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kwa msaada wa kuchepusha mto  uliobadili uelekeo wake  kutokana na mvua nyingi zilizonyesha Mwaka huu zikiambatana na kimbunga HIDAYA na kusababisha  uelekeo wa Mto kuelekea katika makazi na mashamba ya wakazi wa Kijiji hicho na kusababisha uharibifu wa mashamba na makazi ya wananchi hao.

Wananchi hao wametoa shukrani hizo Julai 26, 2024 kwa TAWA kupitia uongozi wa Pori la Akiba Selous Kituo cha Kingupira kwa kutoa mashine inayosaidia kuchepusha mto huo kutoka makazi ya watu, jambo ambalo wamekiri kuwa litasaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao.

Salum Kassim ambaye ni  mkazi wa Kijiji cha Ngarambe amesema mvua kubwa zilizonyesha Mwaka huu ambazo ziliambatana na kimbunga HIDAYA zilisababisha athari kubwa kwa wakazi wa Kijiji hicho kama vile kuharibu makazi yao kwa kubomoa nyumba, kuharibu majengo ya shule na vyoo vya shule  hasa baada ya Mto kubadili uelekeo wake kutokana na kujaa maji mengi.

Salum anasema kutokana na ushirikiano mzuri na ujirani mwema baina ya Kijiji hicho na Pori la Akiba Selous , waliomba msaada  TAWA kupitia  uongozi wa Kituo cha Kingupira kilichopo  katika Hifadhi hiyo na uongozi huo kukubali kutoa mashine ambayo inaendelea kufanya kazi ya kuchepusha mto ili kuokoa maisha na mali za wananchi hao.

Kaimu Kamanda wa Pori la Akiba Selous ambaye pia ni msimamizi wa Kitengo cha ujirani mwema, Jimmy Mshana amesema Kijiji cha Ngarambe ni majirani wa Hifadhi hiyo ambao wamekuwa na ushirikiano nao wa muda mrefu katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuhifadhi hivyo baada ya kuona wamepata changamoto hiyo walilazimika kutoa msaada wa haraka ili kuweza kuwaokoa kwa kuchepusha mtu huo ili wasije wakapatwa madhara makubwa zaidi.

Amesema kazi ya kuchepusha mto huo imefanyika kwa ushirikiano mkubwa kupitia viongozi mbalimbali wa Kata na Kijiji husika pamoja na wananchi wote kwa ujumla.

TAWA imekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi waishio pembezoni mwa Hifadhi mbalimbali inazozisimamia nchini kupitia progamu za ujirani mwema jambo ambalo limewafanya wananchi hao wajivunie uwepo wa Taasisi hiyo katika maeneo yao.

 Ikumbukwe kuwa mapema Mwaka huu TAWA ilitoa misaada mbalimbali ikiwemo vyakula na magodoro kwa wananchi wa wilaya ya Rufiji waliopatwa na mafuriko pamoja kuwapa elimu ya namna ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko.

Comments

Popular posts from this blog

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

HUU HAPA MWENENDO WA KIMBUNGA "HIDAYA" , UPEPO KUVUMA KWA KASI YA KILOMITA 130 KWA SAA

NHIF YAFANYA MABORESHO YA KITITA CHA HUDUMA ZA MATIBABU, YAENDELEA KUPOKEA MAONI