SERIKALI YAJIPANGA KUTOKOMEZA MAGONJWA YASIYOPEWA KIPAUMBELE
Na Mwandishi wetu Dar
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria ifikapo 2030 kutokomeza maambukizi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwenye halmashauri zote nchini humo ili kuwakinga wananchi wake na magonjwa hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya Jenister Mhagama amesema wanatarajia hadi kufikia mwaka 2027 wawe wamevuka asilimia 95 kuelekea kutokomeza magonjwa hayo pamoja na kufanya vizuri licha ya kuwepo changamoto mbalimbali ikiwemo fedha.
Amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto ya kupambana na magonjwa yasiyopewa kipaumbele, Serikali ya uingereza imekuwa ikiisaidia wizara ya Afya, ambapo leo wamekutana na mkamwana wa mwana mfalme wa Uingereza ili kujadili magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwemo mabusha, matende na vikope (Trachoma)
"Leo tumekutana na huyu mke wa mtoto wa mfalme ili kuonyesha maeneo ambayo tumefanya vizuri, kwani Shirika la Afya duniani linataka ifikapo mwaka 2030 tuwe tumeshapambana na magonjwa haya yameondoka katika nchi zetu,”amesema Mhagama.
Amesema Serikali ya Uingereza imesaidia katika sekta ya afya kuanzia mwaka 1998 ambapo walitoa kiasisi cha zaidi ya Sh11.8 bilioni ambazo zimesaidia kusomesha wataalamu,tufanya upasuaji na kwenye magonjwa ya Kikope ambayo yanaweza kusababisha upofu.
Ameongeza kuwa, fedha hizo zimesaidia kununu vifaa tiba vinavyohusiana na macho ambavyo vimepelekwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili,KCMC na Mvumi kama kituo cha sayansi tiba.
“Yapo magonjwa mengine ambayo tumekuwa tukifanya nao kazi kama matende, mabusha,minyoo na tumefanya kampeni ambazo zinatusaidia kuthibiti magonjwa hayo ikiwemo kufanya usafi,kunawa uso na kunawa mikono,”amesema na kuongeza .
Kwa upande wake, Meneja Mpango wa Taifa wa Kuthibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbeke ,Dk Clara Mwasusu, amesema mwaka 2012 Serikali ilianza kutokomeza ugonjwa wa Kikope kwenye halmashauri 69 ambapo wananchi wanaoishi kwenye maeneo ambayo hatarishi wamekuwa wakiwezeshwa dawa.
Dk Mwasusu amesema mwaka huu wameweza kutokomeza ugonjwa huo kwenye halmashauri 60 kati ya hizo tisa bado wanaugua ambapo matarajio yao ifikapo mwaka 2017 wanatarajia kutokomeza ugonjwa huo.
“Watu 167 waliathirika na ugonjwa wa Kikope na tuliwafanyia upasuaji ili kuwakinga na upofu wa kudumu na hivi sasa tumebakiwa na wananchi zaidi ya 10 milioni ambao wapo kwenye halmashauri 20 kati ya hizo 16 wanaendelea kupatiwa huduma,”amesema
Amezungumzia ugonjwa wa Kichocho bado ni tatizo kwa sababu hawajaweza kuudhibiti kwa vile ipasavyo wanatarajia Serikali na mahusiano mazuri ya nchi ya Uingereza watafikia malengo ya kutokomeza ugonjwa huo.
Dk Mwasusu amesema wanatarajia kuanza utekelezaji wa huduma ya bima kwa wote wananchi wa hali ya chini wataweza kupata hiozo huduma kwa kuwa gharama yake ni kubwa wanatakiwa kulipia kuanzia Sh250,000 hadi Sh 300,000
Comments
Post a Comment