ACT WAZALENDO WATOA DOSARI HIZI ZOEZI LA UCHUKUAJI NA UREJESHAJI WA FOMU

 

Na Mwandishi wetu, Dar 

Chama Cha ACT Wazalendo kimesema licha ya mazingira mazuri yanayotangazwa na Serikali kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa kuwa wa huru na haki lakini bado kuna mambo yanayoendelea ili kukwamisha vyama vya upinzani wasiweze kushiriki uchaguzi huo ambapo dosari kadhaa wamezibaini kwa baadhi ya maeneo ambapo wagombea wao wameenda kuchukua fomu .

Akizungumza na waandishi wa Jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti Bara ACT Wazalendo Isihaka Mchinjita amesema katika baadhi ya maeneo wagombea wa ACT Wazalendo nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa  wametakiwa ili wapewe fomu ni lazima wapeleke vitambulisho vya uraia ili kuthibitisha uraia wao vinginevyo hawapewi fomu.

“ Matukio kama haya yamejitokeza katika kata ya Kandawale, kijiji cha Mtumbei Mpopera kilichopo katika jimbo la Kilwa Kaskazini mkoani Lindi, zipo kasoro nyingi ambazo zimekuwa zikitokea katika hatua hii ya kuchukua na kurejesha fomu, ACT Wazalendo tunaamini kuwa matukio haya hayatokei kwa utashi wa wasimamizi wasaidizi wenyewe bali kwa maelekezo, 

"Tunazo taarifa kuwa baadhi ya Wakuu wa wilaya wameagizwa kuhakikisha kuwa ACT Wazalendo haashindi vijiji na mitaa katika uchaguzi huu na tumekuwa tunafuatailia kwa karibu juu ya mwenenndo wa uchaguzi, viashiria vinaonesha ukweli kuhusu taarifa hii na hasa katika mitaa ya jiji la Dar es salaam, kutokana na sababu hizo ACT Wazalendo tunataka hatua  zichukuliwe"amesema Mchinjita.

Aidha, kutokana na changamoto hizo zilizojitokeza kwa baadhi ya maeneo Chama hicho kimemtaka Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI awaondoe wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yote yaliyoripotiwa kuwa na matatizo  ambapo wagombea wao wameahindwa kuchukua fomu ili uchaguzi uende sawa kama ambavyo Serikali inawaaminisha watanzania, uchaguzi utakua huru na haki.

Ameongeza kuwa katika siku chache zilizobaki wagombea wa vyama vyote wachukue na kurudisha fomu bila ya kuwekewa vikwazo na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi maeneo ambayo wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi hawakutoa fomu au kuwa na mgombea  mmoja kwa sababu ya wengine kuzuiwa makusudi kuchukua fomu uchaguzi wa maeneo hayo usifanyike mpaka watakapohakikisha waliojitokeza kugombea kwa mujibu wa sheria na kanuni wamepatiwa haki hiyo ya kugombea.

Sambamba na hayo amesema miongoni mwa dosari zinazodaiwa kujitokeza kwenye mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uchaguzi wa serikali za mitaa ni pamoja na wagombea kunyimwa fomu ambapo maeneo mengi wanachama  wa ACT Wazalendo wanaojitokeza kwenda kuchukua fomu za kuomba uteuzi, wasimamizi wa uchaguzi wamekuwa kwa makusudi wakiwapa nakala moja tu ya fomu na kuwataka waende wakatoe photocopy wenyewe, jambo hilo limetokea katika meneo mengi ya jimbo la Arumeru Mashariki

"Kutakiwa kutoa photocopy kwa mtazamo wetu kuna lenga kwanza kuwapotezea vipato vyao kwa kuwa nakala za fomu za kugombea ni nyingi zinazotakiwa kwa wagombea wa eneo la kijiji husika lakini pia waweze baadaye kuwawekea pingamizi kwamba fomu za uteuzi haziwezi kuwa zilizotolewa copy hivyo zionekane ni nakala za kugushi"

Ameongez, "Ili wawaengue kirahisi, wasimamizi kukimbia ofisi na kutopatikana kabisa kwa lengo wa kuwakimbia wagombea; tukio hili limetokea katika maeneo mengi sana baadhi ya maeneo ni pamoja na Newala vijijini katika kata ya Nandwahi, kijiji cha Nandwahi ambapo msimamizi wa uchaguzi alipoona wana ACT wamefika ofisini kwake kwenda kuchukua fomu aliwaomba wamsubiri kidogo na alichokifanya ni kutorudi kabisa ofisini siku hiyo na siku ya pili tarehe 29 Oktoba"

"Taarifa tuliyonayo ni kwamba msimamizi huyo amehamisha familia yake na yeye hajapatikana ofisini mpaka sasa, pamoja na juhudi za viongozi wetu kuwasiliana na msimamizi wa uchaguzi wa kata na wilaya, hakuna ufumbuzi wa jambo hilo uliopatikana mpaka sasa” Amesisitiza Mchinjita

Amesema kuwa kadhia ya wasimamizi kufunga ofisi ipo katika jimbo la Tandahimba, kata ya Mdimba katika vijiji vya Mpelepele, Minjale, Chitenda na Mdimba. Kata ya Mkwedu katika vijiji vya Matale, Mnyambachi, Tengulengu na Mkwedu, vilevile katika jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza kwenye kata ya Mabatini, mtaa wa Nyerere B ambapo msimamizi wa uchaguzi amefunga ofisi na kupelekea wagombea wa ACT Wazalendo kushindwa kuchukua fomu huku wasimamizi kudai wameshatoa fomu kwa wagombea wa ACT wakati si kweli, tukio hilo limejitokeza Katika jimbo la Tunduma, kata ya Chapwa mtaa wa Chapwa A.

"Msimamizi msaidizi wa uchaguzi ndugu George Enock Sinkolongo amempatia fomu ya kugombea Uenyekiti wa mtaa wa Chapwa A mtu ambaye hajatambulishwa na chama kuwa mgombea wake na hivyo kudai kuwa ACT wamechukua fomu, lakini ukweli ni kuwa mgombea wa ACT Wazalendo aliyeteuliwa na chama ni ndugu Emmanuel Mwawalo huyu amenyimwa fomu mpaka sasa” 

Aidha," tumefanya juhudi ya kuwasiliana na Mtendaji wa mtaa husika ndugu Mariam Lawrence Mwampashi baada ya kujua kuwa anazungumza na viongozi wa ACT Taifa akasema hawezi kuwasikiliza na kukata simu"amesema Mchinjita

Hata hivyo ACT Wazalendo imewaagiza wananchi pale ambapo wagombea wa vyama vingine wamezuiwa au kufanyiwa hila wasishiriki uchaguzi huo, wabebe jukumu la kuhakikisha wanatumia nguvu ya umma kuzuia uchaguzi katika maeneo hayo haufanyika mpaka kasoro hizo zirekebishwe.

Comments

Popular posts from this blog

HUU NDIO USHAURI WA TMA KWA SEKTA HIZI ...

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI