KAWAIDA ATOA UJUMBE HUU SIKU YA UKIMWI DUNIANI


Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2024, Chagua Njia, Tokomeza UKIMWI

Ujumbe wangu, Mohammed Ali Kawaida, _Mwenyekiti UVCCM Taifa

Leo, tarehe 1 Desemba 2024, Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani. Maadhimisho haya yanayoratibiwa kitaifa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), mwaka huu yanafanyika mkoani Ruvuma yakibeba kauli mbiu yenye nguvu na matumaini: “Chagua Njia, Tokomeza UKIMWI.”

Kauli mbiu hii haizungumzii tu mbinu za kujikinga, bali inatufundisha kuchagua njia ya maisha yenye afya, mshikamano, na uwajibikaji ili kufanikisha lengo la dunia la sifuri tatu: sifuri maambukizi mapya ya VVU, sifuri unyanyapaa na ubaguzi, na sifuri vifo vinavyotokana na UKIMWI.

Mimi Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, ninatoa wito kwa vijana wenzangu wa  Kitanzania kushikamana na kutumia nafasi yetu ya kipekee katika mapambano haya. Ni wakati wetu kuchukua hatua, si tu kwa faida yetu binafsi, bali kwa kizazi kizima na taifa kiujumla.

Ukubwa wa Changamoto na Nafasi Yetu Vijana

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu milioni 39.5 wanaishi na VVU duniani kote, huku takriban 1.3 milioni wakipata maambukizi mapya mwaka jana 2023. Ripoti zetu Tanzania zinaonyesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 bado wanakabiliwa na maambukizi kwa viwango vya juu zaidi.

Je, changamoto hii ni ya kushindikana? Hapana. Kwa kuwa sehemu kubwa ya jamii yetu ni vijana, nguvu, maarifa, na uthubutu wetu vinaweza kuwa chachu ya mabadiliko. Hali ya UKIMWI inaweza kubadilishwa ikiwa tutakuwa sehemu ya suluhisho kwa kuchagua njia sahihi na kuhakikisha ujumbe huu unawafikia wote.

Mchango wa Vijana: Nguvu ya Mabadiliko

1. Kuelimika na Kueneza Elimu

Elimu ni silaha kubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Shirika la UNAIDS linatambua kuwa elimu sahihi inaweza kupunguza maambukizi mapya kwa zaidi ya nusu. Vijana tuna fursa ya kutumia majukwaa kama mitandao ya kijamii, vikundi vyetu, na vikao vya kijamii kueneza elimu kuhusu VVU/UKIMWI, njia za kinga, na umuhimu wa kupima afya mara kwa mara.

2. Kujitokeza Kupima na Kutafuata  Matibabu sahihi

TACAIDS inakadiria kuwa asilimia kubwa ya maambukizi mapya yanaweza kuzuilika endapo watu watajitokeza kupima afya zao mapema na kufuata matibabu kwa wakati. Vijana tunapaswa kuwa mstari wa mbele si kwa kuwaelimisha wengine tu, bali pia kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kupima afya zetu na kuhimiza wengine kufanya hivyo.

3. Kupambana na Unyanyapaa na Ubaguzi

Unyanyapaa bado ni kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya UKIMWI. Kwa mujibu wa UNAIDS, zaidi ya watu milioni 8 duniani bado hawapati matibabu kwa sababu ya unyanyapaa. Hili ni jukumu letu vijana kuibomoa dhana hii kwa mazungumzo ya uwazi, mshikamano, na kukubali kuwa UKIMWI sio hukumu ya maisha, bali hali inayoweza kudhibitiwa.

4. Kuchagua Njia Sahihi

Kuchagua njia bora za maisha ni silaha muhimu. Hii inajumuisha matumizi sahihi ya kinga, uaminifu katika mahusiano, na kuepuka tabia hatarishi. Shirika la CDC linasisitiza kuwa matumizi ya kinga kwa usahihi yanaweza kupunguza maambukizi mapya kwa zaidi ya asilimia 95.

Sisi Ni Kizazi cha Mabadiliko

Katika harakati za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, vijana tuna nafasi kubwa. Dunia na Taifa inatutegemea kama kizazi cha sasa kuhakikisha tunaondoa kabisa janga hili. Hii ni fursa ya kuandika historia ya kizazi chetu kwa vitendo vyetu leo.

Wito kwa Vijana wa Kitanzania

Katika siku hii muhimu, nawasihi vijana wenzangu kuchukua jukumu letu kwa dhati. Kama WHO inavyosema, “Ending AIDS is not just a public health goal; it is a moral and social imperative.”

Tukumbuke kuwa kila hatua tunayochukua leo, iwe ni kuchagua kinga, kuelimisha wengine, au kupinga unyanyapaa, inachangia kufanikisha ndoto ya Tanzania isiyo na UKIMWI. Maamuzi yetu ya leo ni zawadi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Comments

Popular posts from this blog

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

HUU NDIO USHAURI WA TMA KWA SEKTA HIZI ...