WAKILI MWABUKUSI AFUNGUKA KUTUPILIWA MBALI MAOMBI YA MDUDE.
Na Mwandishi wetu, Dar
Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imetupilia mbali maombi ya mawakili wa upande wa utetezi kutaka mwanaharakati Mdude Nyagali afikishwe mahakamani kwa madai kuwa kiapo kinzani hakijathibitisha kujeruhiwa na kushikiliwa kinyume cha sheria kwa mwanaharakati huyo.
Mawakili Boniface Mwabukusi na mwenzake Philip Mwakilima, walieleza hoja za mwanaharakati Mdude Nyagali Mpaluka kushikiliwa kinyume cha sheria na kwamba mpaka sasa bado yuko mikononi mwa Polisi hivyo pia walikuwa wakiiomba mahakama iamuru mwanaharakati huyo afikishwe mahakamani.
Hata hivyo Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya aliyekuwa akisikiliza maombi hayo Musa Pomo ametupilia mbali maombi hayo akisema upande wa waleta maombi (Wakili Mwabukusi na Mwakilima) hawajathibitisha kuwa Mdude Nyagali alipigwa wala kujeruhiwa jambo ambalo linaelezwa na mawakili wa utetezi kuwa halikuhitajika na upande wowote mbele ya Mahakama na kama kungehitajika uthibitisho wa vielelezo wangewasilisha ikiwemo mlalamikaji (Mdude Nyagali) kufika mahakamani kueleza madhira yaliyomkuta.
Kwa upande wa mashtaka shauri hilo lilikuwa likiendeshwa na wakili Lodgard Eliaman na wakili Dominic Mushi huku waleta maombi wakiwa ni wakili Boniface Anyisile Kajunjumele Mwabukusi na mwenzake Philip Mwakilima ambapo akizungumza baada ya kutupiliwa mbali kwa shauri hilo Wakili Mwabukusi amesema hawakubaliani na maamuzi ya Mahakama kuu hivyo watajadiliana kuona namna bora ya kufanya kwasababu wanaamini Mdude Nyagali alipigwa na anashikiliwa kinyume cha sheria.
Itakumbukwa kwamba mwanaharakati na mwanachama wa CHADEMA Mdude Nyagali Mpaluka alikamatwa Novemba 22, 2024 huko Mbozi mkoani Songwe pamoja na uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa waliokuwa kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa akituhumiwa kwa makosa kadhaa ikiwemo kutoa lugha za matusi na kujeruhi ambapo tangu kukamatwa kwake aliendelea kusalia mikononi mwa Polisi hadi tunakwenda mitamboni jumatatu hii hivyo mawakili Boniface Mwabukusi na Philip Mwakilima wanaishinikiza mahakama iwaamuru wahusika kumfikisha mahakamani mwanaharakati Mdude Nyagali ikiwa ana kosa lolote badala ya kuendelea kumshikilia jambo linalokinzana na sheria za mwenendo wa makosa ya jinai.
Comments
Post a Comment