RC CHALAMILA ATOA WIKI MBILI WAMACHINGA KUFUNGUA NJIA


Na Mwandishi wetu 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa agizo kwa wafanyabiashara wadogo (machinga) waliopo katika eneo la Kariakoo kuhakikisha wanafungua njia ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia Mei 28, 2025, ili kuruhusu shughuli za kibiashara kufanyika kwa ufanisi kuelekea uzinduzi wa soko la Kariakoo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, RC Chalamila amesema soko hilo limekamilika kwa asilimia 98, hivyo ni muhimu njia za kuingilia kwenye soko ziwe wazi ili kurahisisha uingizaji wa bidhaa.

Amesisitiza kuwa, Serikali itawaondoa machinga waliopo kwenye njia na kuwapeleka kwenye maeneo maalum yaliyotengwa, kama ilivyoelekezwa na Wizara ya TAMISEMI.

Aidha, RC Chalamila ameeleza kuwa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao kwenye soko la awali kabla ya kuungua, watarudishwa kwenye maeneo yao baada ya uhakiki, kwa mujibu wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesisitiza kuwa watahitajika kujaza mikataba, kujiandaa kulipa kodi, na kufuata taratibu mpya za upangaji zinazotumia mfumo wa kidijitali. Ameongeza kuwa mfumo huo umeondoa udalali uliokuwa ukiwakwamisha wafanyabiashara wengi.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Ashrafu Abdulkarim, amesema shirika linaendelea kuratibu urejeo wa wafanyabiashara wa awali katika soko hilo jipya. Kati ya wafanyabiashara 1,520 waliokuwa hapo awali, 1,159 tayari wamejisajili katika mfumo wa kidijitali na kujaza fomu.

Ameongeza kuwa maeneo ya wazi yaliyosalia yatatangazwa rasmi kupitia mfumo wa TAUSI kwa ajili ya kupata wapangaji wapya.

Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam katika kuhakikisha mazingira bora ya biashara na kurudisha hadhi ya Kariakoo kama kitovu cha biashara nchini.

Comments

Popular posts from this blog

HUU NDIO USHAURI WA TMA KWA SEKTA HIZI ...

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI

MAANDALIZI YA MKUTANO MKUU CCM YASHIKA KASI