TFS YAPONGEZWA KWA KUTANGAZA HISTORIA NA MAZINGIRA BAGAMOYO





Na Mwandishi Wetu 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe Shaibu Ndemanga, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi nzuri ya kuendeleza utalii wa kihistoria na uhifadhi wa mazingira, akibainisha kuwa juhudi hizo zimechangia kuongeza pato la wananchi na kuvutia wageni wilayani humo.

Mhe. Ndemanga ametoa pongezi hizo leo Juni 25, 2025 wakati wa mapokezi ya Mjumbe wa Bodi ya TFS, Bi Piencia Kiure, aliyekuwa katika ziara ya siku ya pili ya kikazi Kanda ya Mashariki kwa kutembelea maeneo ya uhifadhi katika wilaya za Bagamoyo (Pwani) na Kinondoni (Dar es Salaam).

“Nawapongeza TFS kwa miradi inayoleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Ukarabati wa maeneo ya kihistoria kama Kaole na Bagamoyo Mjini Mkongwe si tu kuwa unahifadhi urithi wetu, bali pia unachochea utalii wa ndani na kimataifa,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Akiwa Bagamoyo, Bi Kiure alitembelea Makumbusho ya Kale ya Kaole na Mji Mkongwe wa Bagamoyo, ambapo alikagua miradi mbalimbali ya TFS ikiwemo ujenzi wa njia za watembea kwa miguu zilizopo Kaole, ukarabati wa ofisi za kihistoria Mjini Mkongwe na maandalizi ya mradi mpya wa uhifadhi wa mikoko Ras-Kilimoni (Kinondoni, Dar es Salaam)

Akiwa katika eneo la Ras-Kilimoni ambalo liko chini ya Wilaya ya Kinondoni, Bi Kiure alielezwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na TFS katika kulinda mikoko, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taasisi hiyo kuimarisha mifumo ya ikolojia ya pwani na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Bi Kiure aliishukuru serikali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ushirikiano wake kwa TFS na kusisitiza kuwa Bodi itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya kihistoria na kimazingira kote nchini.

“Ushirikiano huu kati ya TFS na serikali za mitaa ndiyo msingi wa mafanikio tunayoyaona leo. Ni wajibu wetu wote kuendeleza maeneo haya kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Bi Kiure.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi  TFS, Dkt. Abel Masota, alibainisha kuwa taasisi hiyo imepokea kwa makini maelekezo na maoni yaliyotolewa na viongozi katika ziara hiyo, na itahakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo alibainisha kuwa wilaya yake ipo katika hatua za awali za maandalizi ya filamu maalum kwa ajili ya kuitangaza Bagamoyo kama kivutio muhimu cha utalii na historia nchini.

Ziara ya Mjumbe wa Bodi ya TFS Kanda ya Mashariki inalenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na utalii, sambamba na kusikiliza changamoto na mapendekezo kutoka kwa wadau wa maeneo husika.

Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI