BENKI YA EQUITY NA SERIKALI KUIMARISHA SEKTA YA MIFUGO NA NGOZI NCHINI
Dodoma – 24 Julai 2025
Benki ya Equity kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanzisha mpango mahsusi wa kuimarisha sekta ya Mifugo na Ngozi nchini, kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya Mifugo, kupanua masoko na kuinua maisha ya wafugaji.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa sekta ya mifugo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Edwin Mhede, alisema serikali imeitaka Benki ya Equity na Bodi yake kushirikiana na serikali kuunda timu maalum ya kitaalamu itakayosimamia uwekezaji katika sekta ya Mifugo.
“Hatua hii inalenga kuboresha ufugaji na mifumo ya uzalishaji wa ngozi, kuongeza ubora na kuifanya sekta hii kuwa chanzo kikuu cha mapato kwa wafugaji,” alisema Dk. Mhede.
Aliongeza pia ili kuboresha Sekta ya Mifugo nchini, hasa kupambana na Magonjwa, Serikali tayari inaendesha kampeni ya kuchanja mifugo yote nchini, ambapo mpaka sasa imechanja zaidi ya mifugo milioni 16, na zoezi hili linatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu, ili kuhakikisha mazao ya Mifugo ikiwemo ngozi yanakidhi viwango vya soko la ndani na kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Equity Group Holdings, Dk. James Mwangi, alisema mpango huu wa ushirikiano na uwekezaji unaendana na dira ya benki ya kuendeleza sekta muhimu za uchumi barani Afrika.
“Tunataka wafugaji wafaidike si kwa kuuza mifugo na ngozi ghafi pekee, bali kwa kushiriki kikamilifu katika minyororo mizima ya thamani. Equity Group ipo tayari kuwekeza katika teknolojia na ufadhili utakaobadilisha sekta ya Mifugo na Ngozi nchini,” alisema Dk. Mwangi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Equity Tanzania, Bi. Isabela Maganga, alibainisha kuwa benki hiyo imejipanga kuwekeza moja kwa moja katika sekta ya Mifugo na Ngozi kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine. Lengo ni kuwawezesha wafugaji, hasa wa vijijini, kupata masoko yenye tija na kuongeza kipato kupitia uboreshaji wa minyororo mizima ya thamani.
“Tumeandaa mikakati ya kifedha na kiufundi kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji kupata mikopo nafuu, kushiriki katika usindikaji na kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi,” alisema Bi Isabela Maganga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Equity, Bw Florens Turuka, aliongeza kuwa sekta ya Mifugo na Ngozi inatoa fursa kubwa za kiuchumi, na akawataka wafugaji kushirikiana na benki kupata mikopo na msaada wa kitaalamu ili kuinua uzalishaji na thamani ya ngozi.
Takwimu za sasa zinaonesha kuwa Tanzania ina ng’ombe takriban milioni 34, mbuzi milioni 24.5 na kondoo milioni 8.5. Sekta ya mifugo inachangia takriban asilimia 7.4 ya Pato la Taifa.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Equity, Bw. Prosper Nambaya, alisema uwekezaji huu ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya Sekta ya Mifugo na uuzaji ngozi ghafi bila usindikaji.
“Kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuunganisha masoko, Tanzania inaweza kuongeza ubora wa Mifugo na thamani ya ngozi zinazozalishwa mara mbili au tatu zaidi, hivyo kuongeza ajira, mapato na mchango wa sekta hii kwenye uchumi,” alisema Nambaya.
Baadhi ya wafugaji walioshiriki mkutano huo walieleza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo, zikiwemo ukosefu wa elimu ya Ufugaji wa Kisasa, uhaba wa malisho na maji, uzalishaji mdogo, miundombinu duni, ukosefu wa mitaji, bima na masoko ya uhakika. Hata hivyo, waliipongeza Benki ya Equity kwa mpango huu, wakisema unaleta matumaini mapya kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Utekelezaji wa ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza ajira kwa wanawake na vijana katika minyororo ya thamani ya Mifugo na Ngozi kuanzia ufugaji, ukusanyaji, usindikaji hadi masoko, sambamba na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la taifa.
Comments
Post a Comment