MIKANDA NANE YA KIMATAIFA KUWANIWA JULAI 26, KNOCKOUT YA MAMA
Na Mwandishi wetu, Dar
Pambano kubwa la Knockout ya mama msimu wa tano inatarajia kuwakutanisha mabondia wenye viwango vikubwa nchini Tanzania, Julai 26, 2025 katika Viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo kubwa litaweka historia kwa kuwa na mapambano nane ya kuwania mikanda mikubwa ya kimataifa ikiwemo ya WBO na WBC.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 24, 2025 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Matangazo na Uzalishaji kutoka Kampuni ya Mafia Promotion Omari Clayton, amesema pambano hilo litakuwa na jumla ya mapambano 10 yakihusisha mabondia wa kimataifa.
"Mapambano nane yatakuwa ya mikanda na lengo ni kufanya "boxing" ya Tanzania iende mbali kimataifa, bondia atakayeshinda atapata fedha, mkanda na nyota, hivyo kutambulika kimataifa," amesema Clayton.
Ameongeza siku hiyo ya pambano itakuwa ni siku ya mtoko kwamba wanataka kila Mtanzania aweze kuifanya Julai 26, 2025 kuwa siku ya Mtoko kwa kwenda kushuhudia pambano hilo.
Naye, Mkurugenzi wa Mafia Boxing Promotion Ally Zayumba akieleza maandalizi ya mwisho kuelekea usiku wa Knockout ya Mama Season 5, ameeleza kuwa kila kitu kipo tayari, na mashabiki wajiandae kushuhudia burudani ya kipekee isiyopimika.
Kwa upande wake, Promota Jay Msangi amewasifia na kuipongeza Mafia boxing promotion kwa kuandaa pambano kubwa linalojulikana kama "Knock Out ya mama."
Ameongeza kwa kusema kuwa uwekezaji waliouweka Mafia boxing promotion ni takribani bilioni mbili na ni uwekezaji mkubwa sana, kwamba mapambano yanayokuja makubwa ya ubingwa ni WBC, WBO, na UBO yote yatafanyika nchini.
Comments
Post a Comment