CCM TUMEDHAMIRIA KUENDELEA KULETA MABADILIKO KATIKA MAENDELEO YA WATANZANIA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Chama kinafanya kazi kubwa ya kuleta mabadiliko ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Aidha, amesisitiza wananchi wandelee kukiamini na kukipa nafasi Chama kiendelee kudumisha amani kwa kuwa maendeleo hayatapatikana iwapo itatoweka.
Wasira alieleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM kutoka Jimbo la Mbeya Vijijini, akiwa katika ziara ya kumwombea kura mgombea urais wa CCM Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani mkoani Mbeya, jana.
Alitumia mkutano huo kumwombea kura Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
"Kazi yetu ni kuleta mabadiliko katika maisha ya watu, maendeleo ni mabadiliko katika maisha ya watu, ukitengeneza barabara unamwezesha huyu mtu aweze kufikisha bidhaa zake sokoni kwa hiyo ataongeza kilimo na uchumi wake utaongezeka kwa sababu ana mahali pakuuza.
"Ukimnyima barabara analima chakula chake cha kula na kufa, anakula ashibe angojee kifo maana hakuna maendeleo hapo," alisema.
Alisema kuwajengea wananchi miundombinu muhimu ikiwemo ya hospitali ni kuwapunguzia safari ya kwenda kutafuta dawa maeneo ya mbali kutoka katika makazi yao.
"Tumepiga hatua lakini maendeleo hayana kikomo na wala maendeleo hayamalizi matatizo yote kwa mpigo kwa sababu hata ukifanya maendeleo makubwa zaidi unaweza ukazalisha matatizo mapya. Hiyo ndiyo dunia, ukilima barabara ya lami speed inaongezeka watu wanakanyagwa halafu unafanya mkutano unaomba waje waweke matuta na wewe ndiye ulikuwa unaomba barabara nzuri ya lami, umeanzisha tatizo jipya.
Comments
Post a Comment