DOYO KUONDOA SHERIA KANDAMIZI YA KIKOKOTOO
Handeni, Tanga
Mgombea Urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, amehutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya Soko la Zamani, Handeni Mjini.
Katika hotuba yake, Mhe. Doyo aliwataka wananchi wa Handeni kutafakari kwa kina changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo tatizo la maji ambalo limekuwa sugu kwa muda mrefu. Mhe. Doyo alisema:
"Tatizo la maji Handeni limekuwepo tangu nikiwa mdogo hadi leo. Chanzo cha maji kiko umbali wa kilometa 50 kutoka Mswaha, lakini maji hayo yamekuwa yakipita hapa Handeni na kuelekea Pangani, kwa sababu tu Waziri wa Maji anatokea Pangani. Hili si jambo la bahati mbaya. Wanahandeni wanapaswa waamke na kuelewa kuwa baadhi ya viongozi siku zote hubeba maslahi yao binafsi. Ukosefu wa maji Handeni si kwa bahati mbaya, bali ni kwa sababu ya kukosa utashi wa kisiasa. Nawaomba mnichague ili twende tukatatue changamoto hii. Wananchi wa Handeni wanahitaji maji kwa haraka na si ahadi tena."
Aidha, Mhe. Doyo aliwahakikishia wananchi kuwa iwapo watampa ridhaa ya kuongoza taifa, atahakikisha wastaafu wote wanapata heshima na haki zao bila kunyanyaswa na sheria zisizo na tija.
"Sheria ya kikokotoo ni kandamizi na inawaumiza watumishi wa umma waliolitumikia taifa hili. Ni dhambi kubwa kwa serikali kuingia mgogoro na wastaafu ambao wametumikia nchi kwa uadilifu. Wastaafu wote wanapaswa kulipwa kwa heshima, na fedha zao kurudi mikononi mwao bila kuchelewa. Nikipewa dhamana ya kuongoza, ndani ya siku 10 baada ya kuapishwa, nitafuta kabisa sheria hii kandamizi. Kila mstaafu atachukua pesa yake kwa uhuru, kwa kuwa hiyo ni amana yake aliyoitumikia katika taifa hili." alisema Mhe. Doyo.
Mikutano ya Mhe. Doyo inaendelea kuvutia mamia ya wananchi kutokana na sera zake zenye maono ya uzalendo, haki, na maendeleo. Msafara wake sasa unatarajiwa kuendelea Manyara na Arusha, huku wananchi wakimsubiri kwa shauku.
Comments
Post a Comment