DOYO, NITAFUNGUA MASOKO UA NJE KWA WAKULIMA WA LUSHOTO



Na Mwandishi Wetu

Lushoto, Tanga

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Mhe. Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake kwa kunadi sera za chama katika eneo la Lukozi, wilayani Lushoto.

Katika mkutano huo uliovuta idadi kubwa ya wafanyabiashara wa mboga mboga, Mhe. Doyo alibainisha changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara hao kuwa ni ukosefu wa masoko ya uhakika. Alieleza kuwa iwapo biashara hiyo itaandaliwa kwa ubora na ustadi, inaweza kuwanufaisha wananchi na familia zao kiuchumi.

“Mazao haya ya mbogamboga yana soko kubwa hata nje ya nchi, lakini tatizo ni kwamba hatujaandaliwa mazingira mazuri ya kibiashara. Kwa sasa mazao yote yanategemea soko moja la Dar es Salaam, na huko nako madalali huwanyonya wakulima. Mkinipa ridhaa, nitahakikisha tunawatafutia masoko ya nje ya nchi. Tutawaleta wanunuzi wakubwa, watasindika mazao yenu na kusafirisha kimataifa. Jiografia ya Lushoto inaruhusu biashara ya mazao haya kufanyika kwa misimu yote,” alisema Mhe. Doyo.

Akizungumza zaidi, Mhe. Doyo aliikosoa serikali iliyopo madarakani kwa kushindwa kuwa wabunifu katika kuwaendeleza wananchi kiuchumi. Alifafanua kuwa sura ya nne ya Ilani ya Chama cha NLD imebeba ajenda ya kilimo, mifugo, uvuvi na usalama wa chakula, akibainisha kuwa takribani asilimia 70 ya Watanzania hutegemea kilimo kama chanzo kikuu cha kipato.

“Tatizo kubwa ni kuwa kilimo chetu kimeendelea kuwa cha mvua na hakina tija. Hata hivyo, ninyi watu wa Lushoto mnabebwa na jiografia ya eneo hili. Changamoto iliyopo ni upungufu wa miundombinu ya kuhifadhi na kusindika mazao,” alisisitiza.

Aidha, aliwahimiza wananchi wa Lushoto kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu na kumpigia kura yeye, Doyo Hassan Doyo, kwa tiketi ya Chama cha NLD, ili kutimiza adhima ya kubadilisha maisha ya wananchi wa Lushoto na Watanzania kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

MWINJUMA AUTAKA UBUNGE KIVULE