“NCHI YENYE MADINI YA KIPEKEE, KUWA NA WANANCHI MASIKINI NI AIBU” DOYO

 


Mwanza, Geita Buseresere 

Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiendelea na kampeni zake Kanda ya Ziwa, amefanya mikutano ya hadhara katika Jimbo la Sengerema, eneo la Stendi ya Zamani, na Kata ya Buseresere, Mkoa wa Geita.

Katika hotuba yake, Mhe. Doyo aliwataka wananchi wa Kanda ya Ziwa kutafakari kwa kina juu ya sababu zinazowafanya kuendelea kukosa maendeleo licha ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kushika dola kwa zaidi ya miaka 60.

Mhe. Doyo aliwaahidi wananchi kuwa endapo watampa ridhaa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atahakikisha wakulima wanapata fursa ya kuuza mazao yao katika masoko yenye tija na faida, badala ya kulazimishwa kuuza katika masoko yanayowanyonya na kuendeleza umaskini. 

“Wananchi, mkiniamini na kunipa kura Oktoba 29, nitasimamia na kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na zenye motisha kwenye mazao yenu yote. Haiwezekani mtumie gharama kubwa katika kilimo chenu halafu mpangiwe bei, hizi ni mbinu za kuendeleza umaskini wenu ili CCM waendelee kuwatawala nyinyi na vizazi vyenu,” alisema Mhe. Doyo.

Aidha, Mhe. Doyo alizungumzia changamoto za miundombinu na huduma za kijamii wilayani Sengerema, akibainisha kuwa licha ya taifa kuwa na rasilimali nyingi kama dhahabu, almasi na tanzanite, bado wananchi wanaendelea kuishi maisha ya umaskini.

 “Nchi hii ina madini ya kila aina, lakini bado wananchi wake hawana maji safi, huduma bora za afya na miundombinu ya barabara. Hili ni jambo la aibu kubwa,” alisisitiza Doyo.

Akizungumzia sekta ya usafirishaji, Mhe. Doyo alisema madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji wamekuwa wakilalamikia gharama kubwa za uendeshaji kutokana na ubovu wa barabara, hali inayosababisha biashara zao kushindwa kuleta faida. Alisisitiza kuwa ni jambo lisilo sahihi kwa serikali kudai kodi kubwa kutoka kwa wafanyabiashara hao bila kuhakikisha uwekezaji kwenye barabara unafanyika ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato.

Mhe. Doyo aliendelea kusisitiza kuwa CCM imeshindwa kutatua changamoto hizi kwa miongo kadhaa, na sasa wanarudi tena kwa wananchi kuomba kura kwa hoja zilezile ambazo hawajawahi kuzitekeleza. Aliibua masuala ambayo yamekuwa kero kwa wananchi wa Sengerema na Buseresere Mkoa wa Geita, ikiwemo, Ubovu wa barabara, gharama kubwa za usafiri, Ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya, Upungufu wa maji safi na salama, Wakulima kushindwa kupata masoko yenye tija kwa mazao yao.

Kampeni za Mhe. Doyo zinaendelea, huku msafara wake ukielekea mkoani Kagera, Wilaya ya Ngara, kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo.

Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

MWINJUMA AUTAKA UBUNGE KIVULE