DOYO: AAHIDI RUZUKU MAALUM KWA WATU WENYE ULEMA­VU

 



Asema: Serikali Ya NLD Itapunguza Kodi Kwa Wawekezaji Ili Kutoa Mitungi Ya Gesi Bure Kwa Watanzania, Ni Hatua Ya Kuokoa Mazingira.

Moshi, Kilimanjaro

Akiwa katika ziara yake ya kampeni mkoani Kilimanjaro, Mgombea Urais wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, amewahakikishia Watanzania kwamba serikali atakayoiongoza itakuwa ya usawa, matumaini na maendeleo kwa kila Mtanzania bila ubaguzi, huku lengo lake kuu likiwa ni kuimarisha usawa wa kijamii na kiuchumi.

Mhe. Doyo amesema wazi kwamba serikali ya NLD itahakikisha makundi maalum nchini yanapewa nafasi na msaada unaostahili. Watu wenye ulemavu, wasioona, wenye ulemavu wa ngozi, na wale wenye changamoto mbalimbali za kimaumbile hawatasahaulika tena iwapo wananchi watamchagua Oktoba 29.

“Serikali yangu itatenga ruzuku maalum kwa watu wenye uhitaji maalum. Tutaanzisha mfumo mahsusi wa kuwasaidia moja kwa moja, bila urasimu, bila foleni, na bila kulazimika kupita kwenye milango ya wizara zisizo na majibu ya haraka kwa watu wenye uhitaji,” alisema Mhe. Doyo kwa msisitizo huku akishangiliwa na wananchi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi sawa ya kuishi kwa heshima, kujitegemea kiuchumi, na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa jipya lenye utu, uzalendo, haki na maendeleo.

Aidha, Mhe. Doyo amesema serikali yake itahakikisha kuwepo kwa utambulisho maalum kwa watu wenye uhitaji maalum, hasa watu wenye ulemavu, sambamba na mikakati maalum ya kitaifa ya kuwapatia makazi, afya bora, elimu ya msingi na huduma za kisaikolojia kwa makundi yaliyo hatarini na yasiyojiweza, kwa lengo la kuimarisha usawa wa kijamii.

“Tunataka Tanzania yenye usawa wa kiuchumi, mazingira safi, na serikali inayosikia kilio cha kila mwananchi. Hii si ndoto, ni dira ya NLD, na mimi nipo tayari kuiongoza Tanzania mpya yenye matumaini kwa wote,” alisema Mhe. Doyo Hassan Doyo, Mgombea Urais wa NLD.

Katika hatua nyingine, Mhe. Doyo amezungumzia kwa nguvu mpango wa kupunguza matumizi ya mkaa nchini kwa kuhamasisha matumizi ya gesi safi ya kupikia.

Amesema serikali ya NLD itapunguza kodi kwa wawekezaji wanaojihusisha na huduma za gesi, hatua ambayo itafungua milango kwa makampuni kutoa mitungi ya gesi bure kwa Watanzania wote na kupunguza gharama ya gesi ili kila kaya iweze kumudu matumizi ya nishati safi.

“Kama baadhi ya kampuni za simu leo zinatoa laini bure, kesho serikali yangu itahakikisha kila Mtanzania anapata mtungi wa gesi bure. Wajibu wako utakuwa ni kununua gesi pekee, kwa bei nafuu! Hii ndiyo njia ya kisasa ya maendeleo, nishati safi, mazingira salama, maisha bora kwa Watanzania wote,” alisema Mhe. Doyo huku akipigiwa makofi.

Ameongeza kuwa mpango huo utasaidia kupunguza gharama za maisha, kulinda misitu, na kuimarisha uchumi wa kaya, kwani familia nyingi zitaokoa fedha walizokuwa wakitumia kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Pia, serikali yake itapiga marufuku ukataji wa misitu bila kibali maalum na kurasimisha biashara ya mkaa, huku Watanzania wakihimizwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.

Mhe. Doyo amesisitiza kuweka mkakati wa kupanda miti milioni 100 katika kipindi cha miaka mitano, ili kurejesha mazingira ya asili, kuhifadhi bioanuai, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mhe. Doyo ameomba wananchi wa Kilimanjaro kumpigia kura, huku akiwashauri kuzingatia ahadi zake tano kuu ambazo amezitoa na kuahidi katika mkoa huo. Ahadi hizo ni Kutoa ruzuku kwa watu wenye uhitaji maalum; kuanzisha mfumo maalum wa usimamizi wa haki na maendeleo ya watu wenye ulemavu; kupunguza kodi kwa wawekezaji katika sekta ya gesi safi; kutoa mitungi ya gesi bure kwa Watanzania wote na kupunguza gharama ya gesi ili kumaliza utegemezi wa mkaa na kulinda mazingira; na kujenga taifa lenye usawa wa kiuchumi na fursa sawa kwa kila raia wa Tanzania.

“Ikiwa serikali yangu aitatekeleza haya ndani ya miaka mitano ya utawala wangu, nipo radhi kutochaguliwa tena, na hiyo ndiyo demokrasia. Chagueni Chama cha NLD, chagueni wabunge na madiwani wa NLD, ili tuwatumikie kwa uwajibikaji na uadilifu mkubwa,” alisema Mhe. Doyo.

Kampeni za Mgombea Urais wa NLD zinaelekea mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, na Zanzibar.

Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

MWINJUMA AUTAKA UBUNGE KIVULE