TMA YATOA MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU NOV 2025 HADI APRIL 2026

 


Na Mwandishi wetu, Dar

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za msimu wa Novemba 2025 hadi Aprili 2026, ikibainisha kuwa maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, hali ambayo inaweza kuathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, hususan katika sekta za kilimo, mifugo, maji, nishati, afya na usalama wa chakula.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus B. Chang’a, amesema mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma, na kusambaa kwenye maeneo ya kusini mwa nchi kufikia Novemba 2025, huku zikitarajiwa kuisha kati ya mwisho wa Aprili na mwanzo wa Mei 2026.

Dkt. Chang’a amefafanua kuwa msimu wa mwaka huu utatawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha, ingawa nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili 2026) inaweza kuwa na ongezeko la mvua ikilinganishwa na nusu ya kwanza, ameeleza kuwa hali hiyo inatokana na mabadiliko ya mifumo ya bahari, ikiwemo joto la Bahari ya Hindi na Atlantiki, yanayoweza kudhoofisha msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kuelekea nchini.

Kwa mujibu wa TMA, upungufu wa mvua unaweza kupunguza unyevu wa udongo, kuathiri ukuaji wa mazao, na kupunguza kina cha maji kwenye mabwawa na mito, hivyo kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani, mifugo na umwagiliaji. Aidha, sekta ya nishati inaweza kukumbwa na changamoto za uzalishaji wa umeme wa maji, wakati sekta ya madini na ujenzi zikitajwa kuwa miongoni mwa zitakazonufaika na upungufu wa mvua kutokana na urahisi wa utekelezaji wa shughuli zao.

TMA imetoa wito kwa wakulima kuandaa mashamba mapema, kutumia mbegu zinazostahimili ukame, kuhifadhi maji na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani. Wafugaji wametakiwa kupanga matumizi ya malisho na maji kwa uangalifu, huku mamlaka za serikali za mitaa zikihimizwa kuboresha mifumo ya mifereji na usambazaji maji safi ili kupunguza athari za mafuriko katika vipindi vya mvua kubwa za muda mfupi.

Dkt. Chang’a amehitimisha kwa kuwataka wananchi na taasisi zote kutumia taarifa rasmi za hali ya hewa kutoka TMA pekee, akisisitiza kuwa ni kosa kisheria kusambaza taarifa za utabiri kutoka vyanzo visivyo rasmi, ameongeza kuwa TMA itaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za mara kwa mara ili kusaidia wananchi kupanga na kulinda maisha yao, mali na shughuli za kiuchumi.

Comments

Popular posts from this blog

MALYA ACHUKUA FOMU YA UDIWANI VITI MAALUM

MAKAMO WA RAIS SMAUJATA ATIA NIA UBUNGE KIVULE

MWINJUMA AUTAKA UBUNGE KIVULE