LONDO - VIPIMO SAHIHI NI MSINGI WA UCHUMI WA VIWANDA NA TEKNOLOJIA
Na Habar Plus
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuimarisha mifumo ya vipimo nchini ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa, kukuza viwanda na kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea sayansi na teknolojia.
Mhe. Londo ametoa kauli hiyo leo Mei 20,2026 jijini Dodoma wakati akifunga rasmi maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani ambapo amesisitiza kuwa maendeleo ya viwanda, biashara na huduma bora hayawezi kufikiwa bila uwepo wa vipimo sahihi na vinavyoaminika.
Amesema serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kisera na kisheria ili kuwezesha biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza ufanisi wa sekta binafsi kwa kuzingatia matumizi ya vipimo vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
“Hakuna biashara yenye uaminifu bila vipimo sahihi, hakuna viwanda vinavyoweza kushindana kimataifa bila mifumo sahihi ya vipimo, na hakuna sera bora bila taarifa sahihi zinazotokana na sayansi ya vipimo,” amesema Mhe. Londo.
Hata hivyo amezitaka taasisi za serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana katika kuimarisha matumizi ya vipimo sahihi ili kuongeza uwazi, ufanisi na uaminifu katika maamuzi ya kitaifa.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yamebeba ujumbe muhimu unaolenga kuonesha namna sayansi ya vipimo inavyoweza kusaidia kujenga imani katika uandaaji wa sera na utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,Mhe. Londo amesema Tanzania haiwezi kufikia uchumi wa viwanda na teknolojia bila kuwa na mifumo madhubuti ya vipimo, maabara za kisasa pamoja na wataalamu wenye ujuzi wa kimataifa.
Amesema vipimo vina mchango mkubwa katika kuongeza tija viwandani, kuchochea ubunifu, kulinda afya za wananchi na kuimarisha biashara ya kimataifa.
“Tunapozungumzia Tanzania ya viwanda, bidhaa zenye ushindani na huduma bora, tunapaswa kutambua kuwa msingi wake ni vipimo sahihi na vya kuaminika,” amesisitiza.
Aidha amesema serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika taasisi za udhibiti na mifumo ya kisasa ya vipimo ili kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa na huduma zenye ubora unaostahili..
Hata hivyo ameutaka Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kuendelea kusimamia haki katika matumizi ya vipimo ili wananchi wapate bidhaa kulingana na thamani halisi ya fedha wanazolipia na kudhibiti udanganyifu katika biashara.
Pia ameliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuendelea kuimarisha maabara za kitaifa, mifumo ya ithibati na ulinganifu wa vipimo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Kwa upande wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), amesema kinapaswa kuongeza programu za mafunzo zinazohusiana na vipimo, tathmini ya ubora na uandaaji wa sera ili kuzalisha wataalamu watakaosaidia kuunganisha sayansi na maendeleo ya uchumi.



Comments
Post a Comment