MWENYEKITI ILALA ATOA MAAGIZO HAYA KWA VIONGOZI KATA YA LIWITI, SEGEREA NA TABATA
Na Mwandishi wetu, HPMedia, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala Said Sidde amewataka Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa wenyeviti wa mashina ili waweze kuwaambia wanachama wao kazi zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan.

Rai hiyo ameitoa alipokuwa katika Mkutano na viongozi wa Kata ya Liwiti, Segerea na Tabata ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake pamoja na kamati ya siasa wilaya kujitambulisha na kuwashukuru wanachama kwa kuwachagua kushika nafasi hizo, na kuahidi wapo tayari kutekeleza majukumu yao hususani katika kipindi hiki cha mkakati wa kufanya kazi za chama ndani ya chama na nje ya chama.
Amesema kuwa, mikakati yao kama viongozi wa CCM Ilala ni kuhakikisha kuwa wanashinda uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 kwa mitaa yote 159 na uchaguzi mkuu 2025 kushinda kata zote 36 na majimbo 3 na kura za ndio kwa Rais Dkt. Samia hivyo uongozi wa wilaya wamefanya vikao na wenyeviti wa mitaa, wabunge madiwani na wakuu wa idara pamoja na Mkurugenzi ili kuainisha maeneo yenye kero na changamoto ili zichukuliwe na serikali kuu na kufanyiwa kazi ikifika kipindi cha uchaguzi mambo yaende vizuri
"Msingi mkubwa wa vikao hivyo tulivyofanya ni maandalizi ya kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu 2025 pamoja na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa inayoendelea kwa sasa hivyo nimpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuondoa zuio la mikutano kwani tunamengi tumefanya ya kuwaeleza wananchi na kuendana na kauli ya raisi ya kujibu hoja kwa hoja na sio matusi"amesema Mwenyekiti Sidde.
Aidha, amewataka viongozi hao kuwa na mahusiano mazuri kujua changamoto zinazowakabili wananchi na jinsi zitakavyotatulia ili wakiwa kwenye mikutano ya hadhara wawe na lakusema kwa wananchi kuwa wametekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, matunda ya vyoo, vivuko na barabara jambo ambapo watakua wametekeleza kwa vitendo agizo la Mwenyekiti wa Chama na Rais Dkt.Samia la kujibu hoja kwa hoja kwenye mikutano ya hadhara.
"Agenda za vyama vya upinzani kuhusu bidhaa za vyakula kupanda itaisha siku si nyingine kutokana na kutolewa kwa mbolea za ruzuku ambazo zitaongeza uzalishaji na agenda za Elimu na Afya tayari CCM imeshatatua kwa kiasi kikubwa hawatakuwa na lakusema na miundombinu ya Barabara inaendelea kutatuliwa "amesema Mwenyekiti Sidde
Sambamba na hayo amesema Viongozi wa mashina ndio msingi wa chama na ndio wenye wanachama hivyo ni vyema kushirikiana nao na uwepo wa mahusiano mazuri baina yao na serikali utawawezesha kujua mambo ambayo CCM imefanya ikiwemo ujenzi wa shule zahanati vyoo na wajue gharama na faida ya miradi hiyo.
Hata hivyo amewaomba viongozi wa mashina ambao bado hawajaunda kamati yao ya watu 4 kuhakikisha kuwa wanaiunda ili kusaidia ufikishwaji wa taarifa mapema toka ngazi za tawi na kumpunguzia mzigo Mwenyekiti na balozi wa shina kutoa taarifa za mikutano kwa wananchi.
Katika hatua nyingine amewaomba Wenyeviti wa mashina kufanya vikao vya mara kwa mara kwani ndio kwenye mizizi ya chama na sehemu ambapo wananchi wanaweza kupeleka kero na changamoto zao zikapelekwa tawini na kutatuliwa na zinaposhindikana kupelekwa ngazi za juu zaidi.
Comments
Post a Comment