DCEA YAMNASA KINARA WA MIRUNGI, YATEKETEZA EKARI 285.5 SAME

Na Mwandishi wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 19 hadi 25 Machi 2025. Katika operesheni hiyo, ekari 285.5 za mashamba ya mirungi zimeteketezwa na watuhumiwa saba (7) wamekamatwa, akiwemo kinara wa biashara haramu ya mirungi nchini aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, Interindwa Zinywangwa Kirumbi, maarufu kwa jina la mama Dangote. Akizungumza baada ya operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo, amesema kuwa, mama Dangote ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini. Kwa zaidi ya miaka 30, amekuwa akiendesha mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hizo za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, licha ya kujua kuwa ni kinyume cha sheria. Aidha, kamishna Lyimo ameongeza kuwa, mwaka juzi Mamlaka ilifanya operesheni wilayani humo na kutoa elimu kwa wananchi ili waachan...