TMA YAELEZEA MAFANIKIO MIAKA MIWILI YA RAIS DKT SAMIA
Na Mwandishi wetu,HPMedia
Imeelezwa kuwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini –TMA kwa ujumla vimeongezeka na kufikia asilimia 88.5, ambapo katika msimu wa mvua za Vuli 2022, viwango vya usahihi vilikuwa asilimia 94.1.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Mamlaka hiyo kuhusu mafanikio ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,imesema hiyo inatokana na huduma za hali ya hewa nchini kueendelea kuboreshwa na kuimarishwa katika maeneo mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya watumiaji Kitaifa na Kimataifa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa viwango hivyo ni juu ya kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70 ambapo ongezeko hilo la usahihi wa utabiri unazifanya huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kuwa za uhakika na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta zote za kiuchumi na kijamii nchini zinazotegemea hali ya hewa.
Mamlaka hiyo imesema itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) katika kutekeleza majukumu ya sekta ya hali ya hewa kwa shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo kufuatlia mabadiliko ya hali ya hewa yanayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.
Vile vile Mamlaka hiyo imefanikiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kukarabati vituo saba (7) vya hali ya hewa vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, Mpanda, Shinyanga, Songea, Mahenge na Tabora pamoja na nyumba tatu za wafanyakazi.
Pia Mamlaka hiyo imeendelea na uboreshaji wa miundo mbinu ya vifaa vya hali ya hewa kuendana na teknolojia na matakwa ya kimataifa ikiwemo kuondoa vifaa vyote vinavyotumia zebaki kwa kununua vifaa 15 vya kidigitali vya kupima mgandamizo wa hewa na vifaa 25 vya kidigitali vya kupima joto hewa.
Kuhusu suala la uboreshaji wa Miundombinu Mamlaka ilinunua Rada nne (4) za hali ya hewa ambapo ufungaji wa Rada mbili (2) katika mikoa ya Kigoma na Mbeya unaendelea. Aidha, utengenezaji wa Rada nyingine mbili (2) kiwandani nchini Marekani umefikia asilimia 63.
Kukamilika kwa Rada hizo nne (4) za hali ya hewa kutakamilisha lengo la muda mrefu la TMA kuwa na Rada saba (7) za hali ya hewa kwa nchi nzima.
Aidha, Mamlaka hiyo imetoa wito kwa wananchi wote kuendelea kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa letu.
Comments
Post a Comment