TIRA NA NBC ZAWAHAKIKISHIA WATANZANIA KAMPUNI ZA BIMA ZINA UKWASI WA KUTOSHA
Na fatma Ally, HPMedia, Dar
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewahakikishia watanzania kuwa kampuni wanazozisimiamia zina ukwasi wakutosha na zinaweza kulipa madai ya bima ambayo yameiva na yanatakiwa kulipwa.
Kauli hiyo imeitolewa jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware wakati akifungua mafunzo ya akaunti ya dhamana kati ya TIRA na Benki ya NBC ambayo yalilenga kuwajengea uwezo wadau wa bima.
Aidha amesema katika kuhakikisha kuwa kampuni za bima hapa nchini zinatumia akaunti ya dhamana katika mabenki ili kuepusha changamoto ya kampuni hizo kutumia fedha bila ruhusa ya Kamishna wa Bima, leo wameanzisha mashirikiano na benki ya NBC.
"Hapo awali kulikuwa na changamoto ndogo ambapo kampuni za bima zilikuwa na kiwango cha fedha katika Benki ya Tanzania (BoT) lakini kiwango hicho huwekwa kwenye hati fungani na zinapoiva zinarudi katika akaunti ya kampuni ya bima hivyo tukawa tunapata changamoto ya baadhi ya kampuni hizi kutumia fedha hizo bila ruhusa ya Kamishna wa Bima "amesema Dkt.Saqware.
Hatahivyo amesema ili kuondoa changamoto hiyo wameanzisha akaunti ya dhamana ambapo benki inapewa masharti na benki itakayoyatimiza masharti hayo wanaanzisha mashirikiano ya kufungua akaunti ya dhamana kama walivyofanya kwa beki ya NBC baaya kuyatimiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema watahakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wateja wao kupitia mfumo wa kieletroniki ambapo Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania itakuwa inafuatilia mwenendo huo.
"NBC ni benki ambayo imekuwepo kwa miongo mitano hivyo tunayo furaha kutoa mafunzo haya kwa wadau wa bima pia Benki ya NBC imejipanga vyema katika kutoa ushauri wa uwekezaji kupitia Idara yetu ya Hazina na Masoko ya Mitaji hivyo nitoe wito kwa makampuni ya bima nchini kuzingatia taratibu zilizowekwa amesema Sabi.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa TIRA Abubakar Ndwata amesema chimbuko la Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni Kanuni ya Bima ya mwaka 2009 inayozitaka Kampuni za Bima kuweka Amana za Usalama angalau 50% ya kiwango cha chini cha mtaji halisi wa kampuni husika ya bima.
Amesema kuwa, TIRA kwa kushirikiana na Chama cha Makampuni ya Bima Tanzania (ATI), walikubaliana kuandaa Mwongozo wa Uwekezaji wa Usimamizi wa Ukwasi ambao pia ulielekeza uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Akiba kupitia benki za biashara ili kuondokana na tatizo la changamoto ya kimtaji au kushindwa kulipa fidia za madai ya wateja wake.
Comments
Post a Comment