SERIKALI YASITISHA UMEZESHAJI WA KINGA TIBA

 


Na Mwandishi wetu, Habari Plus, Dar

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesitisha kampeni za umezeshaji wa kingatiba ya ugonjwa wa Matende na Mabusha katika maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na kufanikiwa kuthibiti magonjwa hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambapo amesema maeneo waliositisha ni pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Ubungo, Temeke na Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam pamoja na kata 10 za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni baada ya kujiridhisha kutokuwa na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Mabusha na Matende katika maeneo hayo.

Aidha amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau hadi sasa imeweza kudhibiti Ugonjwa wa Matende na Mabusha (ngirimaji) katika Halmashauri 112 kati ya 119 na kubakiwa na Halmashauri saba nchi nzima.

"Ugonjwa wa Matende na Mabusha (ngirimaji) ni miongoni mwa changamoto kubwa za kiafya zinazoathiri wananchi katika maeneo hatarishi dhidi ya ugonjwa huu nchini, hapo awali maambukizi makubwa ya ugonjwa huu yalikuwa na katika Halmashauri 119 nchini ambapo watu milioni 31.2 walikuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya vimelea vya ugonjwa huu" amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo, ametaja Halmashauri zenye maambukizi mapya ya ugonjwa huo kwa hivi sasa kuwa ni Pangani, Mafia, Kinondoni, Kilwa, Lindi Manispaa, Mtama na Mtwara-Mikindani ambako kuna jumla ya wakazi 1,203,359.

Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri Ummya amebainisha kuwa mnamo Machi na Agosti mwaka jana na Februari mwaka huu, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa huo na Halmashauri za Manispaa ya Kigamboni, Manispaa ya Ubungo, Manispaa ya Temeke, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Kinondoni walifanya zoezi la tathmini ya kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo katika halmashauri hizo.

"Kwamba matokeo ya tathmini hiyo yanaonyesha kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni na Manispaa ya Ubungo hazina maambukizi mapya ya ugonjwa huo kwa kipindi cha miaka sita (6) baada ya kusitisha umezeshaji wa Kingatiba katika Halmashauri hizo"amesema Waziri Ummy.

Ameongeza kuwa, kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Manispaa ya Temeke na Kata 10 za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambazo ni Bunju, Kawe, Kunduchi, Mabwepande, Makongo, Mbezi Juu, Msasani, Mbweni, Wazo na Mikocheni kwa sasa hazina maambukizi mapya ya ugonjwa wa Matende na Mabusha.

Sambamba na hayo, amesema matokeo ya tathmini hiyo yanaonyesha Kata 10 za Manispaa ya Kinondoni ambazo ni Tandale, Kijitonyama, Mwananyamala, Kigogo, Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi, Hananasifu, Kinondoni na Makumbusho bado zina maambukizi mapya ya ugonjwa wa Matende na Mabusha kwa kiwango cha asilimia 2.3.

Hata hivyo, amesema kutokana na matokeo hayo Wizara ya Afya imesitisha kampeni ya umezeshaji wa Kingatiba ya ugonjwa wa Matende na Mabusha katika maeneo husika ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo hayana maambukizi mapya.

“Maeneo haya ni Jiji la Dar es Salaam, Manispaa ya Temeke na Kata 10 za Manispaa ya Kinondoni. Maeneo haya yanaungana na Manispaaa ya Kigamboni na Ubungo ambazo tulisitisha kampeni za umezeshaji Kingatiba ya Matende na Mabusha mika sita (6) iliyopita,” amebainisha Waziri Ummy.

Amesema kuwa, zoezi la kampeni za umezeshaji wa Kingatiba ya ugonjwa wa Matende na Mabusha katika Kata 10 za Manispaa ya Kinondoni ambazo ni Tandale, Kijitonyama, Mwananyamala, Kigogo, Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi, Hananasifu, Kinondoni na Makumbusho ambapo zoezi hilo litaendelea angalau kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo kabla ya kurudia tena kufanya tathmini.

Comments

Popular posts from this blog

NLD YAZINDUA KAMPENI "FYEKA CCM", YATOA WITO HUU KWA TAMISEMI

TMA YATOA TAHADHARI KUHUSU UWEPO WA KIMBUNGA "HIDAYA"

HUU NDIO USHAURI WA TMA KWA SEKTA HIZI ...