BONGO MOVIE WAFUNGUKA RAIS DKT SAMIA KUWAPELEKA NJE YA NCHI KUJIFUNZA
Na Mwandishi wetu,HabariPlus, Dar
Wasanii wa Filamu za maigizo (BONGO MOVIE) wamempongeza Rais Dkt Samia Suluh Hassan kwa kuwajumuisha kwenye ziara yake ya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza jambo ambalo litafungua fursa mbalimbali kwa wasanii hao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Taasisi ya Ongea na Mwanao Steve Nyerere amesema kuwa jambo analolifanya Rais Dkt Samia ni mfano wa kuigwa kwani anatambua mchango wa kila sekta nchini.
Amesema kuwa, wao kama wasanii watahakikisha wanaitumia fursa hiyo katika kujifunza, kulinda maadili na kuitangaza Tanzania vizuri kiutamaduni na kiutalii jambo ambalo litaivuta Dunia kuifahamu vyema Tanzania.
Hata hivyo Nyerere amewatahadharisha wanasiasa kuwa wasije kusema kwamba jambo analolifanya Rais Samia kuwa ni kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu kupitia kwa wasanii.
Amesema kuwa, Rais Samia anafanya hivyo kama mzazi anayepaswa kuwakumbatia watoto wake wote, ambapo ameleza kitendo cha Wasanii kupelekwa nje kujifunza kitawasaidia kuwainua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Waigizaji Tanzania Chiki Mchoma amesea kuwa kitendo hicho cha Rais Samia kinakwenda kuimarisha Tasnia ya Filamu Tanzania.
Aidha wasanii hao wametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwa Tasnia nzima ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Awali, Rais Samia alitoa kauli yake ya kuanza ya kuwajumuisha Wasanii mbalimbali kwenye ziara zake rasmi nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi juu ya tasnia hizo hivi karibuni alipohudhuria hafla ya uzinduzi wa Albamu ya Staa wa Muziki wa Bongo Fleva Hamarmonize aliyoiita "Muziki wa Samia".
Comments
Post a Comment