Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na Wakulima, Wafugaji, Mamlaka za wanyamapori , Mamlaka za maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta husika ili kujiepusha na athari za mvua zinaponyesha.
Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 31,2024 Jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa mvua za Msimu wa Novemba, 2024 hadi Aprili 2025.
Amesema kuwa, mvua za msimu ni mahususi katika maeneo ya Magharibi mwa nchi Kanda ya kati, Nyanda za juu kusini Magharibi kusini, ukanda wa Pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro ambapo maeneo hayo yanapata msimu mmoja kwa mwaka.
Aidha, kutokana na mifumo ya hali ya hewa, mvua za wastani hadi chini wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida, na Dodoma, huku juu ya wastani zikitarajiwa katika mikoa ya Njombe,Ruvuma,Mtwara,maeneo ya kusini na Magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.
"Mvua nyingi zinatarajiwa katika kipindi Cha nusu ya pili ya msimu kuanzia mwezi February hadi April kwa mwaka 2025, ikilinganishwa na Nusu ya kwanza mwezi Novemba 2024 hadi Januari 2025"
Aidha, vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha kutuama kwa maji, kuongeza mtiririko na kusababisha mafuriko ambayo yanaweza kupelekea uharibifu wa miundombinu na tishio la usalama wa maisha na mali, hivyo mamlaka za miji zinashauriwa kuboresha na kuimarisha mifumo ya maji taka na safi mijini ili kupunguza athari za mafuriko.
Hata hivyo, amesema jamii imeshauriwa kutibu maji ya kunywa, kuzuia na kuharibu mazalia ya mbu, kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo, kuendeleza tabia ya kunawa mikono Kwa sabuni na maji tiririka na kudumisha usafi wa mazingira kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Katika msimu huo wa mvua kubwa kutokea na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi ambayo yanaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu mazingira kupoteza mali na madhara kwa binadamu, hivyo idara ya Menejment ya msaada nchini inashauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yatakayojitokeza.
Hata hivyo, wadau WA sekta binafsi wanashauriwa kushirikiana na wataalam mbalimbali ikiwemo watalaam wa Hali ya hewa ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza, Taasisi za benk na bima zinashauriwa na kutoa huduma mahususi Kwa wadau ili kujenga ustahamilivu katika biashara.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkurugenzi mkuu huyo wa TMA amesema kuwa Mifugo na Uvuvi katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, wafugaji na wavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho, maji na chakula cha samaki.
Hata hivyo amesema milipuko ya magonjwa ya mifugo kama vile homa ya bonde la ufa, ugonjwa wa miguu na midomo, na kuzaliana kwa wadudu wadhurifu kunaweza kujitokeza.
Pia amesema upungufu wa mvua hasa katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2024 hadi Januari, 2025) unatarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji na malisho ya mifugo na kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
"Wafugaji wanashauriwa kuweka mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo,wafugaji na wavuvi wanashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kuzingatia ushauri unaotolewa na maofisa ugani ili kupunguza athari zinazoweza kutokea na kunufaika na hali ya hewa inayotarajiwa."amesema Dr.Chang'a
Comments
Post a Comment