SERIKALI YAONGEZEKA MASAA 24 YA UOKAJI WALIOANGUKIWA NA GHOROFA KARIAKOO
Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Thobias Makoba, amesema zoezi la uokoaji wa watu walionasa kwenye jengo lililoporomoka Jumamosi ya Novemba 16, 2024 Kariakoo kwenye Mtaa wa Congo na Mchikichi Jijini Dasr es Salaam, litaendelea tena kwa saa 24 za ziada baada ya saa 72 za kawaida za kiwango cha kimataifa kumalizika.
Bw. Makoba ameyasema hayo leo novemba 19, 2024, wakati akizungumza na waandishi wa habari Kariakoo kwenye eneo la tukio, ambapo amesema kuongezeka kwa saa hizo 24 za ziada, ni agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alilolitoa kupitia kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, katika kikao cha tathmini kuhusu zoezi hilo la uokoaji ambapo amelitaka jeshi la zimamoto na uokoaji, kuendelea na shughuli hiyo ili kunusuru uhai wa watu ambao bado wamekwama kwenye jengo hilo.
“Tukiwa kwenye kikao cha tathmini cha kazi inayoendelea, moja ya ajenda iliyozungumzwa ni kuhusiana na utaratibu wa uokoaji, kulianza kutokea maneno kwenye mitandao ya kijamii kwamba baada ya masaa 72 kwa kawaida kwa viwango vya kimataifa, zoezi la uokoaji kwenye maeneo kama haya linabadilika, na wanaanza kutumia mashine pale inapolazimu,
sasa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan muda huu ametoa maelekezo kupitia kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, na maelekezo hayo yaje kwa kikosi chetu cha Zimamoto na Uokoaji kwamba zoezi hili liendelee kwa saa zingine 24 za ziada, ni kwamba wasisitishe, kabla ya kubadili hatua yoyote, kwa hiyo zoezi hili linaendelea, halitasitishwa kama ambavyo wananchi wengine wameanza kuwa na hofu” amesema Bw. Makoba.
Amesema lengo ni kuhakikisha maisha ya watu walioko kwenye jengo hilo yanalindwa na kwamba hakuna kifusi kitakachowaangukia.
“Imempendeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba, tutaendelea kutumia mbinu ambazo zilikuwa zikitumika za weledi na ustadi zaidi katika kuhakikisha kwamba, kwanza tunaridhika kwamba hakuna ambaye aliyepo hai atasumbuliwa au ataangushiwa kifusi huko chini, au kwa namna yoyote ile itamkuta ili kumsababishia kupoteza maisha, baada ya masaa 24 tutatangaza utaratibu unaofuata” amesema Bw. Makoba.
Zoezi la uokoaji wa watu walionaswa kwenye jengo lililoporomoka linaendelea kwa kasi kubwa kwa siku ya nne sasa ambapo Serikali inafanya jitihada zote kuhakikisha hakuna madhara yatakayowapata watu walionasa kwenye jengo hilo.
Comments
Post a Comment