AFARIKI AKIWA SAFARINI AKITOKEA MWANZA KWENDA DAR
Na Lilian Kasenene, Morogoro
KIJANA aliyefahamika Godfrey Mbaga anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka (25-30)mkazi wa Mwanza amefariki Dunia wakati akisafiri akitokea mkoa wa Mwanza kuelekea Dar es Salaam kwa basi la Dragon mali ya kampuni ya Ally's.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama alisema tukio hilo limetokea Februari 23, 2025 majira ya asubuhi eneo la Mikese Wilaya ya Morogoro na kwamba alipanda basii lenye namba za usajili T 433 EBG.
Mkama alisema marehemu wakati wakiwa safarini walipofika eneo la Mikese abiria huyo alianza kujisikia vibaya na kufikishwa hospitali kwa matibabu lakini hakupata nafuu na hatimaye alifariki dunia.
Alisema mwili wa marehemu Godfrey umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospital ya rufaa mkoa wa Morogoro kusubiri ndugu wa marehemu kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi.
Wakati huo huo Februari 24, 2025 majira ya asubuhi katika eneo la Cape town mtaa wa Kambi tano kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro ulipatikana mwili wa mtoto anayefahamika kwa jina la Ester Isaya Banzi (10) mwanafunzi wa darasa la tano shule ya msingi Juhudi akiwa ameshafariki.
Kamanda Mkama alisema awali, Februari 23, 2024 zilitolewa taarifa za kutoonekana kwa mtoto huyo katika kituo cha Polisi Kihonda na jitihada za kumtafuta zilifanyika hadi alipopatikana akiwa anaelea juu ya dimbwi la maji.
Alisema uchunguzi wa kubaini chanzo cha kifo hicho umeanza, mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha maiti katika hospital ya rufaa mkoa wa Morogoro.
Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro limetoa wito kwa ndugu jamaa na marafiki wanaomfahamu marehemu aliyefariki kwenye basi wafike kutambua na kuchukua mwili kwa hatua za mazishi.
Kamanda Mkama aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zutakazo saidia kubaini sababu au kifo cha mtoto Ester.
Comments
Post a Comment