SHIGONGO AFUNGUKA MAZITO KUHUSU BUCHOSA, AMPA MAUWA YAKE DKT SAMIA
Mbunge wa Jimbo la Buchosa, wilayani Sengerema Erick Shigongo amesema ana kila sababu ya kumpongeza na kumshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan Kwa maendeleo makubwa aliyoyafanya jimboni kwake.
Akizungumza na waandishi wa habri leo jijini Dar es Salaam Mbunge huyo amesema Rais Dkt Samia amefanyia mambo makubwa ikiwemo kugusa sekta zote muhimu ikiwemo afya, elimu, maji ambapo huduma zote hizo hapo awali ilikua ngumu kupatikana kwake.
Amesema kuwa, yeye amekua ni shuhuda namba moja kwa maendeleo hayo kwani alikua akitembea umbali wa kilomita tisa kwenda na kurudi shule ambapo kwa sasa kadhia hiyo imebaki historia.
"Ndani ya miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, mimi kama mbunge wa Jimbo la Buchosa nimepokea zaidi ya bilioni 62.3 ambapo tumejenga barabara, Sekondari mpya 8, Zahanati 21 vituo vya Afya 5, hilo linatosha kusema kwamba Serikali ya Dkt Samia anawapenda wanabuchosa"amesema Shigongo.
Amesema pamoja na kuyumba kwa uchumi wa dunia baada ya janga la ugonjwa wa COVID-19 lakini Tanzania imepambana kurejesha uchumi wake kufikia asilimia 5 ambapo hapo awali ulishuka kutoka asilimia 6 hadi kufikia asilimia 3 na kwa sasa ni moja ya mataifa yenye uchumi mzuri hivyo watanzania wana kila sababu ya kujivunia uchumi wao.
Ameongeza kuwa, Tanzania ni nchi tajiri sana kwa rasilimali ikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe,madini ya almasi,tanzanite na madini mengine huku katika sekta ya utalii ikiwa ni nchi ya pili duniani baada ya Brazil huku ikiwa namba 1 kwa Afrika nzima katika sekta ya utalii.
"Nataka niwambie Tanzania ni nchi tajiri sana duniani kwa gesi asilia ni nchi ya 82, makaa ya mawe ni nchi ya 50, Dhahabu ni nchi ya 22, Almasi ni nchi ya 10 na Tanzanite ni nchi ya 1 huku upande wa utalii ikishika nafasi ya pili duniani "
Ameongeza "Hivi karibuni nilizungumza kule New York,Marekani kuwa Afrika ni bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali lakini imeshindwa kubadilisha rasilimali hizo kuwa fedha lakini kwa uongozi bora wa nchi yetu Tanzania,Sasa tunatumia utajiri wetu kujiletea maendeleo na Rais Dkt Samia ameamua kutumia utajiri huo kuanza na sekta ya utalii ambao kwa Sasa unaingiza fedha nyingi na pia anaitumia sekta ya Kilimo katika kukuza kipato"amesema.
Amesema watanzania wanatakiwa kumuunga mkono Rais Dkt Samia kwa kuhakikisha wanashiriki vyema katika kuchangia Pato la Taifa (GDP) kupitia sekta mbalimbali za uchumi ili kuendelea kukuza uchumi Wetu na kuongeza kuwa kama Tanzania itaenda kama ilivyo hivi Sasa basi baada ya miaka 15 itakuwa ni miongoni mwa mataifa tajiri zaidi duniani.
Akizungumzia kuhusu mipaka ya kibiaashara Afrika, Shigongo amesema ni wakati wa bara hilo kuamka na kuwa wamoja huku akilitolea mfano Taifa la Marekani ambalo halina mipaka kwenye majimbo yake kibiashara hivyo ni wakati kwa waafrika kuwa kitu kimoja kwa kukataa kuchonganishwa na nchi za Afrika zifanye biashara zenyewe kwa zenyewe na kuepuka kutumia fedha nyingi kuagiza bidhaa kutoka nje.
''Ukienda Marekani ukapanda ndege kutoka New York kwenda Jimbo lingine huhitaji viza na biashara zinafanyika kwa ushirikiano mkubwa lakini Afrika hatufanyi hivyo kwa hiyo ni wakati wetu Sasa kuamka na kukataa kuchonganishwa"
Comments
Post a Comment